Mpelelezi wa doria mtandaoni asimulia alivyobaini ujinai kauli ya Lissu

Dar es Salaam. Shahidi wa pili wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameieleza Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam jinsi alivyobaini jinai katika maneno aliyoyatamka Lissu.

Shahidi hiyo, Mkaguzi wa Polisi John Kaaya amesema ndiye aliyeiona na kuipakua picha mjongeo (video clip) inayomuonyesha Lissu akitamka maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini.

Shahidi huyo anatoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni, Dawati la Doria Mtandaoni kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Dar es Salaam.

Amesema wakati anaiona video hiyo Aprili 4, 2025 ilikuwa imeshatazamwa na watu 39,000 na maoni 300.

Pia amesema wakati anaipakua Aprili 7, 2025, idadi ya watu waliokuwa wameitazama ilikuwa imeongezeka na kufikia watu 52,000 ingawa idadi ya maoni ilibakia ileile 300.

Kaaya amebainisha hayo wakati akitoa ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema, leo Alhamisi 9, 2025.

Kesi hiyo inasikilizwa na majaji watatu, Dunstan Ndungiru, akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika ushahidi wake Kaaya amesema siku hiyo wakati anafanya doria mtandaoni aliona video hiyo katika mtandao wa YouTube wa Jambo TV ikiwa na kichwa cha habari: “Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia majimboni, no reforms, no elections njia panda.

Amedai kuwa baada ya kutazama na kuifungua na kusikiliza, alibaini baadhi ya matamshi yenye viashiria vya jinai, hivyo alimjulisha mkuu wake wa Kitengo, aliyemwelekeza aende kumtaatifu SSP George Bagyemu (kwa sasa ACP), naibu mkuu wa upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam.

Amesema Bagyemu alimtaka aipakue hiyo video na akafanya hivyom kisha akaiweka kwenye flash disk ya GB 8 akampelekea Bagyemu.

Shahidi huyo ataendelea kesho Oktoba 10 kuhojiwa maswali ya dodoso na mshtakiwa Tundu Lissu.

ACP Bagyemu alivyohitimisha

‎Mapema, Shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, ACP Bagyemu amehitimisha ushahidi wake wa siku nne, akisisitiza kuwa uchochezi wenye lengo la kuitisha Serikali ni kitendo cha uhaini.

Shahidi huyo, ambaye ni Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (DZCO), ametoa maelezo hayo kwenye majibu yake ya kusawazisha ushahidi wake na majibu yake ya maswali ya dodoso aliyoulizwa na Lissu.

Bagyemu amewasilisha ushahidi wake kwa siku nne mfululizo kuanzia Jumatatu, Oktoba 6, 2025 na kuhitimisha leo Alhamisi, Oktoba 9, 2025 mbele ya majaji watatu, Dunstan Ndunguru, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2)(d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kutokana na maneno aliyoyatoa kuhusu kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga kujibu hoja zilizotokana na maswali ya Lissu, Bagyemu amebainisha kuwa kuzuia uchaguzi kwa kufuata utaratibu wa kisheria si kosa, bali kuzuia uchaguzi kwa njia zisizo halali zenye vitisho na uvunjaji wa sheria, ndiko kunakoweza kuhesabika kama uhaini.

Akitoa ushahidi wake leo, shahidi huyo ametumia dakika 27 kujibu hoja za kusawazisha zilizoibuliwa wakati wa mahojiano yake na Lissu, kisha akaruhusiwa kuondoka baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakamani haukuwa na maswali zaidi.

Baadhi ya hoja alizojibu Bagyemu wakati akiulizwa maswali ya kusawazisha na Wakili Katuga, zilihusu tafsiri ya matamshi ya kuzuia uchaguzi na athari zake kisheria.

‎Wakili: Uliulizwa kufanya uchochezi ni kosa la uhaini, ukajibu ndio ni kosa la uhaini, hapa ulimaanisha nini? Fafanua.

‎Shahidi: Kufanya uchochezi kwa nia ya kutishia Serikali ni uhaini si tu neno uchochezi peke yake.

‎Wakili: Ulionyeshwa hati ya mashtaka na kuonyeshwa maneno na ukaulizwa neno Serikali lipo humo? Wewe ukasena neno kama Serikali halipo, ila kimaudhui lipo, sasa tunataka ufafanua uliposema majibu hayo ulimaanisha nini?

‎Shahidi: Neno Serikali kimaudhui kwenye hii hati ya mashtaka limo. Ukiangalia haya maneno na ukiangalia msimamo huu ni uasi, uchaguzi upo kwa mujibu wa Katiba na sheria, hivyo ukiangalia neno kama neno halipo, ila ukiangalia kimaudhui neno Serikali limo.

‎Wakili: Pia uliulizwa kuhusu neno kuzuia uchaguzi, ni kosa la uhaini? Ukatujibu kuwa kuzuia uchaguzi kiuhalali sio kosa la uhaini, sasa hapa umetuacha, wafafanulia majaji.

‎Shahidi: Kuzuia uchaguzi kwa kufuata utaratibu sio kosa la uhaini. Bali kuzuia uchaguzi kwa njia zisizo halali, kwa vitisho na kuvunja sheria zilizopo, ni uhaini

‎Wakili: Shahidi uliulizwa maswali mengi kuhusu maelezo ya P (shahidi), uliulizwa nani aliyechapisha maudhui hayo mtandaoni, ukajibu ni P, na baadaye ulivyoulizwa tena ukasema ni P na Tundu Lissu, sasa tunaomba utufafanulie, ulimaanisha nini?

‎Shahidi: Tundu Lissu kwa kitendo chake cha kuongea na waandishi wa habari, alikusudia maneno yake yachapishwe mtandaoni.

‎Shahidi: Mtu wa Jambo TV yeye ni mwandishi wa habari, mwenyekiti wa Chadema alikuwa anaongea nao kwa lengo la maneno hayo yachapishwe mtandaoni.

‎Wakili: Shahidi kuna swali pia uliulizwa, chama cha upinzani kuipinga Serikali kwa njia halali sio kosa, ulimaanisha nini hapa? Wafafanulie majaji

Shahidi: Chama cha upinzani kupinga Serikali kwa njia halali sio kosa, ila ni kosa kama watafanya kwa vitisho.

‎Jana katika mahojiano yake na Lissu, shahidi huyo aliulizwa maswali mbalimbali kuhusu ushahidi wake wa msingi alioutoa kuhusiana na shtaka linalomkabili, huku akitumia fursa hiyo kueleza simulizi ya wasifu wake.

Katika simulizi hiyo ya wasifu, Lissu aliwasilisha kwa mtindo wa kujieleza kisha akimuuliza shahidi iwapo anafahamu hivyo au la.
ACP Bagyemu, katika majibu yake, baadhi ya sentensi alikiri kufahamu, zingine akasema anafahamu kwa sehemu, mengine akasema hayajui na mengine kuyakanusha.

Kuhusiana na maelezo ya wasifu aliyokuwa akihitimisha kwa kumuuliza shahidi kama anafahamu, Lissu alijikita katika harakati zake za kupigania demokrasia na haki za watu, lakini shahidi alidai hafahamu harakati hizo wala hajui kama ni mtu muhimu.

Maelezo mengine yalihusu nyadhifa na tuzo alizowahi kupata ndani na nje ya nchi kutokana na harakati zake, lakini shahidi huyo alidai hafahamu kama mshtakiwa alipata tuzo.
Baada ya ACP Bagyemu kumaliza kutoa ushahidi wake, alianza kutoa ushahidi shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri, Mkaguzi wa Polisi, John Kaaya (45) kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandaoni.