Mwinyi aahidi kuboresha elimu kuwajengea vijana uwezo wa ushindani kimataifa

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema iwapo atarejea madarakani kwa kipindi cha pili, ataendelea kuwajengea uwezo vijana kwa kuwapatia elimu bora ili wahimili ushindani ndani na nje ya nchi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Oktoba 9, 2025 Tunguu, Kusini Unguja wakati akizungumza na vijana wa vyuo vikuu na makundi mbalimbali ya vijana ikiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za urais za kukutana na makundi mbalimbali.

Amesema akipata ridhaa ya kuwaongoza tena Wazanzibari atahakikisha kuwa anafanya kila linalowezekana kuendelea kuongeza bajeti ya elimu, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na wale wa ngazi ya stashahada.

“Ninyi vijana ndiyo viongozi na ni kundi muhimu sana mbapo zaidi ya asilimia 65 ya wapiga kura wote ni vijana hivyo ni lazima mjengewe uwezo ili mpate elimu bora,” amesema.

Amesema Serikali ya awamu ya nane ilipoingia madarakani bajeti ya sekta ya elimu ilikuwa ni Sh80 bilioni, lakini mpaka sasa bajeti ya Wizara ya Elimu imepanda hadi kufikia Sh864 bilioni.

“Kwa hivyo, kipaumbele cha kwanza tulichotoa ni elimu kwa sababu tunataka vijana wetu katika nchi hii waelimike,” amesema.

Akizungumzia bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, Dk Mwinyi amesema ilikuwa ni Sh13 bilioni lakini hadi kufikia mwaka 2025, bajeti hiyo imepanda hadi kufikia Sh37 bilioni.

Hivyo, amesema ndiyo maana vijana wanaopata mikopo wamefikia 20,000 kutoka vijana 8,000 waliokuwa wakipata mikopo hiyo.

Aidha, amesema Serikali ilifanya uamuzi ya makusudi ya kutoa mikopo kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya stashahada ambapo tayari vijana 3,500 wa diploma ambao wanapata mikopo ya Serikali.

“Yote haya yanaonyesha kipaumbele tulichokiweka katika elimu lakini kwa kutambua kwamba tunawajengea uwezo vijana tunapowapa elimu,” amesema.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwajengea uwezo katika elimu kuanzia ngazi zote sambamba na kuendelea kuvijenga vyuo vya mafunzo ya elimu ya amali ili vijana wanaokosa kuendelea katika elimu ya juu basi waweze kupata elimu ya ufundi.

Amesema, kundi la vijana lina umuhimu wa kipekee katika kufanya maamuzi au hatma ya uongozi nchini kwa sababu idadi kubwa ya wapiga kura visiwani Zanzibar ni vijana ambapo zaidi ya asilimia 65 ya wapiga kura ni vijana.

Amesema, serikali ya Chama cha Mapinduzi inatoa upekee maalumu kwa masuala yote yanayohusu vijana na kwamba wanachotaka vijana ni kupata fursa ambapo fursa hizo zipo katika maeneo matatu ambayo ni elimu, ajira na fursa ya uongozi.

Aidha Dk Mwinyi aliwahakikishia vijana hao kuwa katika awamu ya pili akipata ridhaa basi Serikali yake itavuka lengo la kuajiri ambapo itatoa ajira zaidi ya 350,000 kwa vijana.

Ameaema, anatambua changamoto hiyo imekuwa ni kubwa kwao na kwamba atahakikisha kuwa vijana wengi zaidi wanapata ajira katika uongozi wake.

Amewahidi kuwapa nafasi nyingi zaidi za uongozi vijana pindi akipata ridhaa ya kuwaongoza tena Wazanzibari na kusema kuwa vijana hawakumuangusha katika awamu yake ya kwanza ya uongozi.

Sambamba na hayo, Dk Mwinyi amewataka vijana kuhakikisha wanawahamasisha vijana wenzao Oktoba 29 kwenda kupiga kura kwani kwa kufanya hivyo ndipo kutakihakikishia ushindi Chama cha Mapinduzi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed amewataka vijana kuhakikisha kuwa wanawahamasisha vijana wenzao kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, 2025.

Amesema vijana wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kuhimizana kuhusu suala zima la amani, umoja na mshikamano kwa mustakabali mpana wa maisha yao ya sasa na ya baadaye.