Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi amesema iwapo akirejea madarakani, Serikali yake itaweka mafungu makubwa ya kukopesha wajasiriamali bila riba ili wakuze biashara zao.
Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 9, 2025 wakati akizungumza na wajasiriamali katika ukumbi wa Abdulwakil, Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Katika awamu hii, tutaangalia namna ya kuwafikia wengi kwa mitaji midogo sio mpaka afungue akaunti, ni kweli mtu hawezi kuwa anauza vitumbua halafu umwambie afungue akaunti,” amesema.
Amesema katika mpango huo, kutakuwa na fedha kutoka Serikali Kuu, fedha kutoka kwa wafadhili na kutoka taasisi za serikali na watakopa fedha nyingi kutoka kwenye taasisi zingine ili kuwakosesha wajasiriamali hao.
“Eneo la mitaji tutaliweka vizuri zaidi ili kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi kuliko ilivyo na kuondoa urasimu ambao umeonekana kwa kiasi fulani,” amesema Dk Mwinyi akiwaomba wamchague tena.
“Tutajipanga vizuri zaidi wafanyabiashara wapate mazingira, tutatengeneza maeneo ili mpate maeneo ya kutosha,” amesisitiza.
Hata hivyo, amesema hawataruhusu kila sehemu ifanyike biashara badala yake kutakuwa na mpangilio maalumu wa kujenga miundombinu hiyo.
“Hii ni moja kati ya dhamira zangu kama tukirudi madarakani, kuwawezesha wajasiriamali,” amesema.
Amesema miongoni mwa wajasiriamali hao wapo wanaojua cha kufanya na mawazo mazuri ya kutoa ushauri kuboresha biashara hizo lakini wanashindwa kuwafikia watendaji hivyo jambo hilo pia litawekwa sawa na kuwahusisha katika kutoa ushauri.
“Kwa hiyo tutategeneza mazingira ili wenye mawazo mazuri wawe wanaishauri Serikali ili kupata mwelekeo mzuri wa kuboresha mazingira ya wajasiriamali,” amesema Dk Mwinyi.
Mgombea huyo, pia, amesema wataendelea kutafuta masoko ya bidhaa za mwani kuwasaidia wajasiriamali wa bidhaa hizo maana wengi wanakosa masoko.
Pamoja na masoko, watainua ili watengeneze viwanda wenyewe ” hapa tunapozungumza viwanda sio lazima kiwe kikubwa na mashine kubwa, kama mtu anaajiri watu 10 hicho kinaweza kuwa kiwanda sisi tutakachofanya ni kuwawezesha waajiri watu wangu zaidi.”
Awali, baadhi ya wajasiriamali wamesema katika masoko yaliyojengwa milango dado ni michache hivyo ipo haja kuongeza mingine na kuwa na urasimu kwenye upatikanaji wa mikopo.
“Tunaomba hii mikopo itufikie zaidi, halafu maeneo mengine dhamana ya kukodisha milango inakuwa kubwa,” amesema mjasiriamali, Khadija Khamis.
Katika hilo, Dk Mwinyi amesema wataliangalia kwani lengo hawajengi masoko ili kupata kodi kubwa bali ni kuwawezesha wananchi.