Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Rahma Mwita ameahidi kukomesha michango isiyokuwa na tija shuleni endapo atakapochaguliwa kushika nafasi hiyo.
Mbali na hilo, Mwita amesema akipewa ridhaa hiyo, atahakikisha idadi ya walimu wa shule za msingi na sekondari wanaongezwa ili kuendana na mahitaji ya wanafunzi.
Ameeleza hayo leo Alhamisi Oktoba 9, 2025 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Hananasif, akisema atahakikisha pia shule mpya zinajengwa sambamba na uboreshaji wa sekta za afya katika jimbo hilo.

Mgombea ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Rahma Mwita ( kulia), akimnadi mgombea udiwani wa Hananasif, Sophia Kaborogo katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika kata hiyo
“Kumekuwa na changamoto au wananchi wa Kinondoni kulalamika kudaiwa michango ya shule isiyokuwa na tija, niwaahidi nitakwenda kulisimamia hili kuanzia katika baraza la madiwani hadi bungeni.
“Wana Kinondoni nipigieni kura Oktoba 29, tukamalize changamoto hii, sambamba na kusimamia uboreshaji wa huduma za afya kupitia mfumo wa bima kwa wananchi.
“Ni aibu kuona watoto wanashindwa kuhudhuria masomo kwa sababu ya michango ya mara kwa mara. Nikipewa dhamana nitahakikisha ada na michango ya aina hiyo zinafutwa ili kila mtoto apate haki ya msingi ya kusoma,” ameeleza Mwita.
Mbali na hilo, mgombea huyo ameahidi kuongeza idadi ya walimu na kusimamia ujenzi wa shule mpya ili kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani, hatua ambayo alisema itainua ubora wa elimu.

“Nitapigania mfumo madhubuti wa bima ya afya utakaomwezesha kila mwananchi kupata matibabu bila kikwazo cha kifedha, sambamba na huduma bure za kujifungua kwa kina mama wajawazito tofauti na hali iliyopo sasa,” amesema.
Mgombea udiwani wa Kata ya Hananasif kupitia ACT-Wazalendo, Sophia Kaborogo amesema wananchi wa kata hiyo wanakabiliwa na kero ya usalama, akisema licha kila mwezi kulipa ada ya ulinzi shirikishi, lakini bado wanadai kuibiwa katika makazi yao.
“Nikishika nafasi hii, nawaahidi nitashirikiana na watendaji wenzagu kuweka mfumo bora na madhubuti wa ulinzi shirikishi unaowajibika kwa wananchi, wenye uwazi, ushirikiano wa kweli, na matokeo yataonekana,” amesema Kaborogo.