Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema ili chama hicho kijihakikishie ushindi wa urais wa kisiwa hicho, ni muhimu Wazanzibari kujitokeza kupiga kura Oktoba 29.
Amefafanua kuwa mafuta (watu wampigie kura) yanahitajika ili safari ya ACT-Wazalendo kuweka historia ya kushika dola ya kuiongoza Zanzibar ikamilike.
Othman ameeleza hayo leo Alhamisi Oktoba 9, 2025 wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika uwanja wa Gamba katika majimbo ya Chaani na Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika hotuba yake, Othman ametumia mtindo wa kuwauliza wananchi wa Chaani kama wanaridhika na mfumo wa maisha ya sasa ya kisiwani ambayo si rafiki kwa Wazanzibari kutokana na kukabiliwa ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira kwa vijana.
Hata hivyo, wananchi hao wa Chaani walimjibu Othman kwamba hawaridhisha na mwenendo wa maisha yaliyovyo, jambo ambalo lilimfanya mgombea huyo kuwaambia akidai Serikali iliyopo haijali maisha yao ndio maana kuna hali ngumu.
“Sisi tumeshasema kazi yetu itakuwa kuwawezesha wakulima na wavuvi ili kujikimu kimaisha, ndugu zangu hayo hamtaki? Hatujachoka maisha haya? Je, hamtaki ufalme katika nchi yenu au maisha ya kuheshimiwa, sasa kama mnataka je tupo pamoja kwenye safari hii?
“Niwaombe jambo dogo safari hii (Oktoba 29), tutafika, lakini mafuta yake ni kura yako. Jamani kura mtampa Othman Masoud,” akijibiwa na wananchi hao kuwa atapewa.
Mbali na hilo, Othman aliwasilisha ombi jingine akisema ili safari ikamilike zaidi Wazanzibari wanapaswa kuwachagua madiwani, wawakilishi na wabunge wanaotokana na chama hicho ili kukamilisha safu bora ya uongozi,” amesema.
Katika mkutano huo, alirejea kauli yake kwamba ACT- Wazalendo, ikishika dola Serikali itakayounda itawatumikia na kuwaheshimu Wazanzibari ili kujisikia faraja kuzaliwa katika kisiwa hicho.
Mjumbe wa Kamati Kuu, ACT-Wazalendo, Juma Duni Haji amesema wananchi wa eneo wamezinduka na kupenda upinzani hasa chama hicho. Amedai kuwa miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini hakuna neema ya maisha nafuu kwa Wazanzibari.
“Tupo kwenye kampeni ya kuleta mabadiliko yanayotakiwa kufanyika na wananchi wa Zanzibar, kilichotuleta hapa ni kuomba kura mpigieni mgombea wa ACT-Wazalendo, (Othman Masoud) maana wagombea urais wapo wengi.
“Othman ana elimu ya kutosha, kwa hiyo elimu Othman yupo vizuri. Ameshafanya kazi katika taasisi mbalimbali pamoja na serikalini, tumpigieni kura za wingi, huyu ndiye mgombea mwenye msimamo kuhusu masilahi ya Zanzibar, mpeni nafasi ya kuonyesha uwezo wa kuendesha Serikali,” amesema Duni maarufu ‘Babu Duni’.