Raia wanne wa kigeni mbaroni kwa kuipeleleza Serikali ya Traore

Ouagadougou. Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imewakamata wafanyakazi wanne wa mashirika yasio ya kiserikali kwa tuhuma za kukusanya kwa siri taarifa nyeti za taifa hilo.

Wafanyakazi hao wamekamatwa baada ya kubainika kukusanya data na taarifa kuhusu serikali ya kijeshi ya taifa hilo ili kuzitoa kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yamekuwa yakiituhumu kwa ukandamizaji na uminywaji wa haki za binadamu, tangu iingie madarakani mwaka 2022.

Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Usalama wa Burkina Faso, Mahamadou Sana imeeleza kuwa waliokamatwa ni wafanyakazi wa shirika la kimataifa la usalama lisilo la kiserikali (INSO) lenye makao yake makuu Uholanzi, linalojihusisha na masuala ya usalama wa kibinadamu.

Amesema miezi mitatu iliyopita, wafanyakazi hao walibainika kukusanya taarifa za serikali na walipigwa marufuku kuendelea na kazi hiyo lakini walikiuka zuio hilo.

“Waliozuiliwa ni pamoja na rais wawili wa Ufaransa, wa Senegal,   wa Czech, Mali na raia wanne wa Burkina Faso ambao tuliwazuia kukusanya taarifa za serikali lakini walikiuka,” amesema Sana.

Ameongeza kuwa taifa lao halitakuwa tayari kurudishwa nyuma na kila mwenye nia ovu na serikali ya sasa inayongozwa na Kapteni Ibrahimu Traore, ambayo imekuwa ikipigwa vita na mataifa ya Magharibi.

Amewakumbusha wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa kutimiza wajibu wao kwa kuheshimu serikali hiyo na kufuata sheria za taifa hilo na miongozo sahihi ya mashirika yao.

Wakati huohuo, shirika la kibinadamu la Uholanzi (INSO) limekataa madai hayo na kueleza kuwa tuhuma hizo za mipango ya uhaini na ujasusi dhidi ya wafanyakazi wake ambao wana lengo la kufuatilia mwenendo wa haki katika serikali hiyo, si za kweli.

Shirika hilo limesema limejitoa kufanya kila kitu ili kuwezesha kuachiliwa huru kwa wafanyakazi wao wanaoshikiliwa na Serikali ya Burkina Faso wakiwa salama.

Ameiomba Serikali ya Burkina Faso kuangalia uwezekano wa kuwaachilia wafanyakazi wake ili waendelee na majukumu yao.

Imeandikwa Elidaima Mangela kwa msaada wa mashirika ya habari.