Samia: Hakuna majaribio katika uendeshaji wa nchi

Bunda. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameonya kwamba hakuna majaribio kwenye uendeshaji wa nchi huku akiwataka Watanzania kukichagua chama hicho ambacho amesema kitafanya kazi na maslahi yao yatapatikana.

Mgombea huyo amewataka wananchi wasikubali kudanganyika, bali wachague chama na watu wanaoaminika kwa kazi ambazo zinaonekana.

Samia amebainisha hayo leo Alhamisi Oktoba 9, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Bunda Mjini mkoani Mara, akitokea mkoani Mwanza alikofanya mikutano minne, kisha akasalimia eneo la Lamadi, Wilaya ya Busega mkoani Simiyu kabla ya kuingia Mara.

Amewataka wananchi kukichagua chake ili kiendelee kuliongoza Taifa hili kwani hakuna majaribio katika uendeshaji wa Serikali. Amewataka wasidanganyike, bali wachague watu wenye uzoefu katika uongozi.

“Katika uendeshaji wa nchi hakuna majaribio unampa nchi yule ambayo unayemuamini ataendesha vyema na maslahi ya wananchi yatapatikana na ukiangalia Tanzania ukiangalia chama ambacho kweli kitafanya kazi na maslahi ya wananchi yatapatikana ni CCM,

“Wengine bado mkiwapa wengine serikali au jimbo wanakwenda kuwafuja, kuwapoteza kwa sababu wakiingia kwanza ni kujifunza lakini utakapompa jimbo asiye CCM, anakwenda kuongea na nani, anaenda kumuomba nani barabara au maji, maana mwenye Serikali ni CCM,” amesema.

Mgombea huyo amesisitiza: “Ndugu zangu wa Bunda, msicheze na hiyo kitu, pelekeni kura kwa wagombea wa CCM ili safari yetu ya maendeleo iendelee, msidanganyike, maendeleo na maslahi yenu yatatokana na serikali ya CCM.”

Mgombea huyo amesema serikali yake itaendelea kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi na miundombinu ambapo wataongeza bajeti kwa Wakala wa Barabara (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ili wajenge barabara zitakazopitika mwaka mzima.

“Hapa Bunda kwenye sekta ya uvuvi tumeleta vizimba 47 vya kufugia samaki na vimeongeza ajira kwa vijana, mabwawa matano ya kufugia samaki na katika ilani yetu ya 2025/30 inatutaka tuongeze nguvu kwenye uvuvi na kuweka viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi pamoja na sekta ya kilimo ikiwemo skimu za umwagiliaji,” amesema mgombea huyo.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wassira, amemtaka mgombea huyo kutokubabaishwa na watu wachache wanaoleta chokochoko kupitia mitandao ya kijamii.

 “Sisi CCM tumeleta mgombea wetu kuomba mumchague na kuirudisha CCM madarakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano, licha ya mazingira aliyoingia nayo Samia, Watanzania wengi walikuwa hawaelewi kitakachotokea lakini Samia alituambia maneno mawili, ‘Kazi Iendelee’.

“Alipewa mtihani mkubwa, aliachiwa miradi mikubwa ikiwemo reli ya kati ikiwa haijakamilika, Bwawa la Mwalimu Nyerere na kwa kipindi kile kulikuwa na tatizo la umeme hadi tukaanza mgao, lakini amefanikiwa kukamilisha miradi yote ya kimkakati,” ameongeza.

Wasira amesema pamoja na mazingira hayo, Samia aliongoza nchi na kuhakikisha umoja wa Taifa unaendelea, amani inakuwepo.

“Ziko chokochoko nyingi na mimi nataka leo niwaambie, chokochoko ziko kwa wachache wanaotumia mitandao ya kijamii, siyo kwa watu wote. Naomba msome mitandao ya kijamii kwa uangalifu.

“Namwambia mgombea wetu ambaye ana nguvu na amefanya kazi kubwa wala asibabaishwe na watu hao wachache, maana kuna watu hata ukifanya mazuri namna gani wananunia hata mafanikio,” amesema.

Kuhusu maendeleo wilayani Bunda, Wasira amesema miaka minne iliyopita, shule 10 mpya za msingi zimejengwa na madarasa 203 huku sekondari zikijengwa shule mpya 15 na madarasa 121, zahanati 20, vituo vya afya vitatu na hospitali ya wilaya ambavyo vimechangia kupunguza vifo vya mama na mtoto.