Bagamoyo. Balozi wa Ufalme wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya bin Ahmed Okeish amesema Serikali ya taifa hilo imeweka dhamira ya dhati ya kuwezesha kilimo cha tende nchini kwa ajili ya lishe, kuimarisha usalama wa chakula, kuboresha maisha ya watu na kukuza uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Balozi huyo ametoa kauli hiyo leo Oktoba 9, 2025 baada ya kutembelea mradi wa kukuza miche ya tende walioufadhili chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI-Mikocheni, eneo la Chambezi, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Tayari miche 3,700 imekuzwa kupitia mradi wa kukuza kilimo cha tende chini ya FAO, ukifadhiliwa na Saudi Arabia na itasambazwa pamoja na vifaa muhimu kwa wakulima zaidi ya 250.
Mbali na wakulima, maofisa kilimo watajengewa uwezo wa namna ya kulima zao hilo na teknolojia mbalimbali kuwezesha uzalishaji wa miche kwa njia ya kisasa.
TARI inaongoza mchakato wa uhimilishaji kwa kuanzisha mashamba ya mfano na kufanya utafiti ili kuhakikisha kilimo cha miwa ya tandi kinafanikiwa katika mazingira ya Tanzania.
Balozi Okeish amesema Ufalme wa Saudi Arabia, kupitia Kituo cha Misaada ya Kibinadamu na Uokoaji cha Mfalme Salman (KSrelief), umejizatiti kikamilifu kusaidia wakulima wa Tanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuboresha tija katika kilimo na kupanua aina ya mazao yanayolimwa katika maeneo yenye ukame.
“Tutaendelea kuwaunga mkono kwa msaada wa kitaalamu na kuwawezesha wakulima, ili Watanzania waweze kuzalisha bidhaa bora za tende,” amesema Balozi Okeish.
Aidha, balozi huyo aliwataka Watanzania kutilia mkazo kilimo cha tende, akibainisha kuwa kilimo hicho kina thamani kubwa nchini Saudi Arabia na kinaweza kubadilisha maisha ya Watanzania katika maeneo yenye ukame wa wastani.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Nyabenyi Tipo Tito, ameipongeza Saudi Arabia kwa msaada wake thabiti, akisema ushirikiano huo umekuwa na mchango mkubwa katika kukuza kilimo endelevu cha tende katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Tanzania, hususan Dodoma na wilaya jirani.
“Tunaishukuru Serikali ya Saudia Arabia kwa namna inavyojitolea, ushirikiano huu umewezesha upanuzi wa mradi huu wa kilimo cha tende,” amesema.
Kwa mujibu wa Fadhili Mtengela kutoka FAO, mradi huo ulianza Januari 2024 na tayari umefikia mafanikio muhimu, ikiwemo ununuzi wa trekta mpya pamoja na vifaa vyake ambavyo vimekabidhiwa kituo cha TARI Hombolo, ambako maandalizi ya mashamba ya mfano yanaendelea mkoani Dodoma.
Amesema katika utekelezaji wa mradi huo, miche 3,000 ya tende yenye ubora wa juu aina ya Ghannami dume, Nawader, Barhi, na Medjool, iliingizwa kutoka India, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), na Misri mwezi Aprili 2025.
Mtengela amesema baada ya miche hiyo kuingizwa nchini, kwa kipindi cha miezi mitatu iliwekwa karantini kwa ajili ya uangalizi na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viwatilifu Tanzania (TPHPA) na kuidhinishwa kwa usambazaji.
“Miche mingine 700 imewasili hivi karibuni kutoka UAE, na kufanya jumla ya miche iliyoingizwa nchini kufikia miche 3,700 ambayo sasa ipo kwenye karantini Chambezi,” amesema Mtengela.
Ingawa kilimo cha tende si kipya kabisa nchini Tanzania, bado hakijatumika kikamilifu. Katika miche iliyoingizwa nchini, kila mti unaweza kutoa kati ya kilo 40 hadi 150 za matunda kila mwaka kwa miongo kadhaa, huku mkulima akipata kati ya Sh 5,000 hadi 10,000 kwa kila kishada cha tende.
Mbali na kilimo, mnyororo wa thamani wa zao hilo kuanzia vitalu vya miche hadi usindikaji na masoko hutoa fursa pana ya ajira na ujasiriamali, hasa kwa vijana na wanawake.
Kwa upande wa mazingira, miti ya tende husaidia kupambana na jangwa, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kurejesha ardhi iliyoharibika; yote haya ni sehemu muhimu ya mkakati wa Tanzania wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa msaada unaoendelea kutoka Saudi Arabia na FAO, Tanzania sasa ipo katika nafasi nzuri ya kuwa mzalishaji tende mkuu wa Afrika Mashariki.