Dodoma/Mbeya. Serikali imewahakikishia wafanyakazi wa Kiwanda cha Wakulima Tea Company (Watco), kilichopo wilayani Rungwe, mkoani Mbeya, kuwa watalipwa stahiki zao na kurejea kazini.
Aidha, imeeleza kuwa kiwanda hicho kinatarajiwa kurejea katika uzalishaji ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.
Hatua hiyo, inakuja baada ya wafanyakazi wa kiwanda hicho kuandamana kwa mabango Oktoba 2, 2025 wakipinga kufukuzwa kazi wakisisitiza kutoondoka kazini hadi kulipwa stahiki zao kiasi cha zaidi ya Sh2.17 bilioni.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na wakulima wa chai kupitia vyama vyama vyao vya ushirika na kampuni ilivyokuwa inaendesha kiwanda hicho.
Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Oktoba 9, 2025 na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao cha kujadili mustakabali wa kiwanda hicho.
Walioshiriki kikao hicho ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chai, Imani Kajura, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo (TPAWU) Mkoa wa Mbeya, Jacline Novat na wawakilishi wa wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Mweli amesema kuwa lengo la kikao hicho ni kujadiliana na kushauriana kuhusu changamoto zilizokikumba kiwanda hicho, ambapo changamoto ya kwanza ni kufungwa kwa kiwanda kwa takribani miezi mitano.
Amesema sababu za kufungwa kwake ni nyingi na zimejadiliwa kwa kina katika kikao hicho.
”Tumekubaliana pamoja na CRDB (Benki ya CRDB) kwa sababu ndiye anayemwezesha kifedha mwekezaji wa kiwanda hiki kuwa kiwanda kifunguliwe ndani ya miezi mitatu ili wakulima waweze kuuza chai ndani ya kiwanda hiki. Na tayari tumeshakubaliana mambo ya kufanya kwa kila upande kuanzia leo ili wakulima ndani ya miezi hii mitatu waanze kuuza chai kwenye kiwanda hicho,” amesema Mweli na kuongeza kuwa;
”Lakini, jambo kingine ambalo tumekubaliana ni kwamba mwezi wa tisa kiwanda hiki ambacho kimefungwa kwa takribani miezi mitano wafanyakazi wake walisitishiwa ajira zao kutokana na kiwanda kutofanyakazi kwa miezi mitano na mwekezaji aliona hana fedha za kuwalipa,” amesema.
Amesema kuwa changamoto iliyowakumba wafanyakazi haikuwa kusitishiwa ajira, bali ni kuhakikisha wanalipwa stahiki zao.
Ameeleza kuwa kikao kilichofanyika leo kimejadili kwa uwazi njia za kuhakikisha malipo hayo yanalipwa, kwa kushirikiana na wawakilishi wa wafanyakazi. Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia suala hilo kwa ukaribu.
Mweli amesema kutokana na majadiliano waliyofanya leo, ana imani ndani ya miezi miwili wafanyakazi wataendelea na ajira kama kawaida kwa sababu wanategemea kiwanda hiki kifunguliwe.
”Kwa hiyo ni imani yangu kusema kuwa Serikali ipo karibu na wananchi na niwahakikishie wananchi wote wa Rungwe wanaozunguka kiwanda hiki kwamba wataendelea kulima na kuuza chai yao kwenye kiwanda hiki kama ilivyokuwa kawaida baada ya kuwa tumemaliza taratibu hizi zote,” amesema.
Amesema Benki ya CRDB imeonyesha utayari wa kutoa fedha kwa mwekezaji huyo au kwa wawekezaji wengine wapya ambao wameshajitokeza ili kuhakikisha kwamba kiwanda kinaendelea na utoaji huduma kwa wananchi na uzalishaji.
Katibu huyo amekitaka chama cha wafanyakazi kuendelea kusimamia haki za wafanyakazi na hakuna haki ya mfanyakazi yeyote itakayopotea.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Mashambani na Kilimo nchini (TPAWU) Jacline Novat amepongeza hatua hiyo akieleza kuwa kilio cha wafanyakazi sasa kimeisha.
Amesema wameona Serikali ilivyowathamini wananchi wake akieleza kuwa kilio cha wafanyakazi hao kwa sasa kimeisha wakisubiri utekelezaji wa maelekezo mengine.
“Tunaipongeza na kuishukuru Serikali kwa kujali na kuthamini mchango wetu, kilio cha wafanyakazi kimesikika hadi kuweza kuingilia kati na kumaliza mgogoro huu,” amesema Jacline.
Naye Meneja wa kiwanda hicho, Obadiah Ngobola amesema kauli ya Serikali wameipokea kwa furaha kwa kuwa hitaji lao ilikuwa ni kupata stahiki zao, hivyo wanaendelea na kazi zao kwa amani.
Amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio na matokeo mazuri kwa kujibu kilio cha wafanyakazi akiipongeza na kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo.
“Kikao kimekuwa cha uamuzi bora, hatukutarajia Serikali kuingilia kati na kuchukulia suala hili kwa uzito, tumefurahi na kushukuru kwa utaratibu kufuatwa kwa kuwa nchi inazo taratibu zake,” Amesema Ngobola.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya madai ya wafanyakazi (WCT), Robert Shayo amesema uamuzi wa Serikali umekuwa wa busara kwa kusikia kilio cha wananchi wake na kuweza kuingilia kati kumaliza changamoto hiyo.
“Sisi msimamo wetu ilikuwa ni kubaki kazini hadi tupate stahiki zetu, ina maana hata leo (jana) wangetupa chetu tungeondoka muda huu huu, kipekee na kwa niaba ya wafanyakazi tunashukuru sana Serikali,” amesema Shayo.