Serikali yahamasisha watumishi wa umma kwenda kupiga kura

Dodoma. Serikali imewahamasisha watumishi wa umma kuhakikisha wanashiriki upigaji wa kura siku ya uchaguzi mkuu ili nao watumie haki yao ya kuchagua na kila mmoja anatakiwa kuwa katika kituo alichojiandikishia.

Hata hivyo, watakaoshindwa kufika katika vituo walivyojiandikisha wanatakiwa kupiga kura mahali walipo kwa kuchagua nafasi ya Rais pekee kwani inaruhusiwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, lakini jambo la lazima ni kwamba kila mmoja akachague.

Wito huo umetolewa leo Alhamisi Oktoba 9, 2025 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Juma Mkomi wakati akizungumza na watumishi kuhusu wiki ya huduma kwa wateja.

Uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unatarajia kufanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 licha ya baadhi ya majimbo na kata kutofanya uchaguzi siku hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo kwa baadhi ya wagombea wa vyama vinavyoshiriki.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora Juma Mkomi

Mkomi amesema Serikali itaruhusu watumishi watakaokuwa na sababu za msingi ndiyo wasafiri lakini wengine kama hawakufanya maboresho kama walivyoagizwa, watalazimika kupiga kura kwa nafasi ya Rais pekee.

“Serikali iliwaagiza watumishi wote kufanya maboresho ya kadi zao, hivyo hatutegemei kuwepo na sababu zingine, hata hivyo kuna watu wamefanyiwa uhamisho hivi karibuni ambao kwa namna yoyote lazima tuwape ruhusa wakapige kura walikojiandikisha,” amesema Mkomi.

Akizungumzia wiki ya utumishi wa umma, amehimiza kuwepo na utumishi uliotukuka ambao utatoa matokeo chanya kwa wananchi wanaowategemea kwa huduma.

Katibu Mkuu huyo amewasisitiza watumishi kote nchini kujiepusha na rushwa kwani wananchi wanaumizwa na vitendo hivyo na wanalalamika.

Amesema huduma bora kwa wananchi zinasaidia kuweka haki na usawa katika utendaji lakini kuiaminisha Serikali kwa wananchi wake na kuwaondolea maswali na hofu ya kiutendaji.

Jana, katika ziara yake katika Wilaya ya Bahi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alihimiza wasimamizi wa vituo na taasisi kuwaruhusu watumishi wao siku ya uchaguzi ili wakapige kura.

Senyamule ambaye amekuwa akitolea mfano wa uchaguzi wa mwaka 2020 kwamba chini ya nusu ya wapigakura katika mkoa wake ndiyo walikwenda kupiga kura jambo ambalo halitoi picha nzuri.

Mgombea udiwani wa Kata ya Ipagala jijini Dodoma kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Danson Kaijage amesema kuhimiza uchaguzi ni jambo jema isipokuwa wengi wanakwenda kwa maelekezo.

Kaijage amesema kila Mtanzania, bila kujali nafasi yake, ni muhimu aachwe kufanya uamuzi wake mwenyewe bila kuelekezwa na kupewa masharti kama ambavyo baadhi ya chaguzi zilishuhudiwa.