Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede amesema bila kuwa na afya imara ya mifugo, Tanzania haitaweza kufanya biashara kwenye sekta hiyo na mageuzi hayatafanikiwa.
Amesema afya ya mifugo ni kigezo mojawapo cha mapinduzi ya sekta hiyo, hivyo Serikali imeanza mkakati wa kuimarisha mifugo kwa kuwapatia chanjo.
Dk Mhede ameyasema hayo leo Oktoba 9, 2025 wakati akifunga mafunzo yanayolenga kuboresha ujuzi wa wataalamu wa mifugo katika kudhibiti magonjwa ya wanyama na kuimarisha afya ya mifugo, mafunzo yanayofadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kupitia mradi wa ISAVET.
“Kwa kutambua haya, tumeanza kutoa chanjo kwa mifugo yenye thamani ya Sh69 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, lengo ni kuchanja mifugo yote na kutokomeza magonjwa 13 tuliyokusudia,” amesema Dk Mhede.
Amesema kichaa cha mbwa, homa ya mapafu, sotoka, midondo ya kuku ni miongoni mwa magonjwa ambayo Serikali imedhamiria kuyadhibiti ili mazao ya mifugo yaliwe bila kuwa na mashaka ya afya zao.
“Mavuno tuliyovuna mwaka uliopita wa fedha ulikuwa ni tani milioni 1.04 za nyama na zililiwa hapa hapa nchini, tani 15,400 ziliuzwa nje ya nchi. Hatuwezi kuacha ziliwe hapa kama hatuna uhakika na afya ya wanyama wetu,” amesema.
Kutokana na umuhimu wa afya ya wanyama, Dk Mhede amesema uwekezaji wa wataalamu ni jambo la lazima ili kuwa na uhakika wa wataalamu watakaoongoza sekta hiyo.
Amesema kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa, sekta ya mifugo ni ya mageuzi na matarajio ya sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa hautafikiwa kama hakutakuwa na wataalamu imara.
Dk Mhede amesema kwa idadi ya mifugo waliopo nchini, mafunzo ya mara kwa mara yanahitajika kwa wataalamu.
Amesema kama ambavyo kuna kiwango rasmi cha daktari mmoja wa binadamu kumhudumia mtu kwenye kituo cha afya, vivyo hivyo ni lazima kuwe na uwiano wa mtaalamu mmoja na kiwango cha mifugo atakachohitajika kuhudumia kwa mwaka ili kuwafikia wanyama hao kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Dk Benezeth Lutenge amesema mafunzo hayo yanayofadhiliwa na FAO yalianza tangu 2018 kwa majaribio hadi sasa, na tayari wataalamu 168 wamepatiwa mafunzo.
Amesema kutokana na utoaji wa mafunzo hayo, kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika kushughulikia magonjwa ya wanyama.
“Tangu tumeanza mafunzo haya tumekuwa tukipata uwakilishi mkubwa kutoka Wizara ya Mifugo, kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Programu hii imechukuliwa kwa umuhimu mkubwa. Tunaendelea kujipanga kuhakikisha mafunzo haya ni endelevu na tunafikia watu wengi zaidi ili kuwa na matokeo,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Zanzibar, Dk Asha Zahran amesema hawakuwa na kitengo cha kufuatilia magonjwa ya mifugo lakini sasa tayari wameanzisha kituo hicho.
Amesema wataalamu waliopewa mafunzo kupitia FAO walikwenda kuwafundisha wengine na sasa kila wiki wanapokea ripoti ya magonjwa ya mifugo katika maeneo mbalimbali visiwani humo.
“Tulikuwa na lengo la uchukuaji wa sampuli, kupitia mafunzo haya kwa miaka miwili tumekuwa tukivuka malengo yetu ya uchukuaji wa sampuli na kujua dawa sahihi ya kushughulikia maradhi ya mifugo,” amesema.
Programu ya mafunzo ya ISAVET (In-Service Applied Veterinary Epidemiology Training) inayofanikishwa na FAO nchini Tanzania, inalenga kuboresha ujuzi wa wataalamu wa mifugo katika kudhibiti magonjwa ya wanyama na kuimarisha afya ya mifugo.
Mafunzo hayo yanahusisha wataalamu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na yanaendeshwa kwa ushirikiano wa karibu na serikali za maeneo hayo mawili.
ISAVET inalenga kuwapatia maofisa wa mifugo ujuzi wa kipekee wa utambuzi, ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya mifugo.
Programu hii ni muhimu kwa kuwa magonjwa ya mifugo yanaweza kuathiri sana uchumi na usalama wa chakula.
Mafunzo yanajumuisha masomo ya darasani na mafunzo kwa vitendo ambapo washiriki wanajifunza mbinu bora za kuepuka na kudhibiti milipuko ya magonjwa ya mifugo.