Simulizi mgombea ubunge alivyouawa Siha

Siha. Mgombea ubunge wa Jimbo la Siha kupitia Chama cha Wananchi (CUF) mkoani Kilimanjaro, Daudi Ntuyehabi, ameuawa na wananchi baada ya kudaiwa kumjeruhi kwa kisu mwenzake, Abdul Mohamed, wakati akiamua ugomvi wa kudaiana fedha.

Kufuatia tukio hilo, familia ya marehemu imesema imepokea kwa masikitiko taarifa za kuuawa kwa ndugu yao na imeiomba Serikali kuingilia kati na kuchukua hatua dhidi ya waliohusika na tukio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Simon Maigwa leo Jumatano, Oktoba 8, 2025, tukio hilo lilitokea usiku wa jana Oktoba 7, 2025, katika Kijiji cha Kilingi, wilayani Siha.

Kufuatia mauaji hayo, watu wanane wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi kwa kumshambulia mgombea huyo hadi kufariki dunia.

Kamanda Maigwa amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni Hamadi Issah Mohamed, Alphonce Kinyaha, Rizik Amedeus, Frank Paulo Lutindi, Shedrack Emmanuel, Jeremia Mnkondo, Zainab Elisha, na Issah Mohamed.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, akibainisha kuwa mauaji hayo yalitokea baada ya mgombea huyo kumchoma kwa kisu tumboni Abdul Issah Mohamed na kusababisha utumbo kutoka nje.

“Mohamed bado anaendelea na matibabu hospitalini, na inadaiwa chanzo cha kuchomwa kisu ni kitendo cha kwenda kuamua ugomvi uliozuka kati ya Daudi Wilbard Ntuyehabi (marehemu) na Hamadi Issa Mohamed wakati walipokuwa wakinywa pombe kwenye grosari, wakigombania fedha walizokuwa wakidaiwa,” amesema Kamanda Maigwa.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linakemea vikali tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi, kwani matokeo yake mara nyingi yamekuwa ni madhara makubwa katika jamii.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwao, dada wa mgombea huyo, Annet Ntuyehabi ameiomba Serikali kuingilia kati akisema wauaji wamekatisha ndoto za ndugu yao aliyekuwa akitaka kuongoza wananachi wa jimbo hilo kupitia nafasi ya ubunge.

“Tunaomba Serikali itusaidie ili waliohusika na mauaji ya ndugu yetu wachukuliwe hatua kali kwani wamekatisha uhai wake angali mdogo na alikuwa akitegemewa na familia,” amesema.

Annet amesema jana usiku walipopata taarifa za mauaji ya ndugu yao, walipatwa na mshituko kwa kuwa bado ni mdogo na ana watoto wadogo, ambao walikuwa wakimtegemea.

“Ilikuwa ni majira ya saa moja kwenda saa mbili usiku, ghafla tukapata taarifa kwamba kuna ugomvi umetokea baina ya kaka (mgombea) na wenzake, kisha wakapigana hatimaye akawa amefariki kaka yangu,” amesema Annet huku akibubujikwa machozi.

Amesema, “Tulikuwa tukiishi na kaka yetu vizuri bila shida yoyote, alikuwa na ndoto zake nzuri za kugombea nafasi ya ubunge kupitia Chama cha Wananchi (CUF).

Amesema kifo chake kimeacha pengo kwa familia kwa kuwa kaka yake alikuwa ni baba wa watoto wawili, mmoja darasa la nne na mwingine darasa la kwanza.

Naye shemeji wa marehemu, Rogate Mwandry amesema kwa sasa hawana cha kufanya, bali wanaiachia Serikali na Jeshi la Polisi wafanye kazi yao ya kufuata sheria.

“Usiku nikiwa Ngarenairobi nilipigiwa simu saa tatu, nikaambiwa shemeji ameshambuliwa na wananachi, nikauliza kwa kisa gani nikaambiwa alikuwa anagombana na wenzake, nilipofika eneo la tukio nikaambiwa amepelekwa hospitali ya wilaya, nikaelekea huko, nilipofika nikaambiwa ameshakufa,” amesimulia shemeji yake huyo.

Amesema kifo cha Ntuyehabi ni pengo kubwa kwa familia hasa kwa watoto wake ambao bado ni wadogo na ameacha mke aliyekuwa akimtegemea sana.

Akizungumzia kuhusu maziko, shemeji wa marehemu, Alpha Mwandry amesema kwa sasa wanasubiri baadhi ya ndugu kutoka Geita kwa ajili ya mipango zaidi.

“Kama familia tupo hapa tunasubiri ndugu zake waje kutoka Geita, ndio tunasubiri wafike ili tuendelee na taratibu nyingine za mazishi,” amesema.

Jirani wa mgombea huyo, Deus Kanje amesema tukio hilo ni la kusikitisha na la kikatili.

“Kifo hiki kimetusikitisha sana, mimi naitazama zaidi familia yake, ameacha watoto bado wadogo sana, lakini mkewe pia, hii ni ngumu sana,” amesema jirani huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Msimamizi wa Uchaguzi jimboni humo, Marco Masue amesema kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uchaguzi mgombea ubunge anapofariki na ikathibitishwa na INEC shughuli za kampeni za ubunge katika jimbo hilo zinasitishwa mpaka itakapotangazwa vinginevyo.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 71 cha Sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani (1) ya mwaka 2024 endapo Msimamizi wa uchaguzi atahakikisha mgombea ubunge amefariki, maana yake atatoa tangazo la kusitisha shughuli za kampeni za mgombea ubunge katika jimbo husika mpaka hapo tarehe nyingine itakapotangazwa,” amesema Masue.

Amesema, “Kwa hiyo shughuli za uchaguzi katika Jimbo la Siha zimesimama mpaka hapo INEC itakapotoa maelekezo mengine.”

Aidha, amesema shughuli za kampeni za Urais na madiwani katika Jimbo hili zinaendelea kama kawaida.

Hili ni jimbo la pili kwa INEC kusitisha kampeni baada ya Septemba 25,2025, iliahirisha uchaguzi wa Jimbo la Fuoni kutokana na mgombea kiti cha ubunge kwa tiketi ya CCM, Abbas Mwinyi kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Lumumba Mjini Unguja.

Abbas aliyekuwa kaka mkubwa wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, alifariki dunia Septemba 25, wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Siku chache baadaye INEC ikatangaza kuwa uchaguzi huo pamoja na udiwani wa kata za Mbagala Kuu Dar es Salaam na Chamwino mkoani Morogoro, utafanyika Oktoba 30, huku fomu za kuomba nafasi hizo zitaanza kutolewa Oktoba 15  hadi  Oktoba 21, 2025.

CUF yatoa pole kwa familia

Akitoa pole kwa familia ya mgombea huyo, Katibu wa chama hicho Wilaya ya Siha, Adam Ramadhan amesema chama kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mgombea huyo.

“Tunasikitika sana kwa tukio lililotokea la kifo cha mgombea wetu wa ubunge Jimbo la Siha, tunaungana na familia katika maombolezo haya, taarifa zaidi tutazipata baadaye kuhusu mazishi yake,” amesema Katibu huyo.