KUNA mjadala ambao unaonekana kuteka vijiwe vingi vinavyojadili soka ukihusu tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi na tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baadhi wanahoji kwa nini Mchezaji Bora wa Mwezi asitokane na miongoni mwa washindi wa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi.
Yaani wale wanaoshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi waorodheshwe pamoja kisha Kamati inayohusika na uteuzi wa washindi wa tuzo itoe mshindi mmoja hapo.
Katika kujadiliana hapa kijiweni tumebaini kwamba sio lazima Mchezaji Bora wa Mwezi atoke katika kundi la wachezaji waliofanikiwa kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.
Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi inatolewa kwa mchezaji ambaye amefanya vizuri katika mchezo husika ambaye inawezekana akashindwa kuonyesha kiwango kizuri katika mechi nyingine za mwezi huo.
Ile ya Mchezaji Bora wa Mwezi inatolewa kwa mchezaji aliyeonyesha uwezo mkubwa katika mwezi mzima. Kwa maana nyingine ni ambaye amekuwa na muendelezo wa ubora katika michezo mingi ya mwezi mmoja.
Inawezekana hakupata tuzo ya mechi katika mchezo fulani lakini akawa alizidiwa kidogo na aliyepata katika mchezo huo kisha akaja kuendeleza ubora katika michezo mingine iliyofuata kwa maana ya muendelezo.
Mfano, mwanafunzi A amefanya mitihani mitatu kwa mwezi. Mtihani mmoja akapata maksi 9/10, mwingine akapata maksi 5/10 na akapata pia makisi 5/10 kwa mwingine. Halafu kukawa na mwanafunzi B ambaye mtihani wa kwanza amepata maksi 8/10 kisha mingine akapata maksi 7/10 na 7/10.
Kiujumla huyo mwanafunzi B ndio atakuwa kinara wa jumla wa mwezi maana japo hakuongoza mtihani mmoja, amekuwa na mjumuisho wa maksi nyingi hivyo ndivyo unavyoweza kufananisha tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi na Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.