:::::::::::;;
Na Mwandishi Wetu, – Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, leo Oktoba 9, 2025, amezindua rasmi programu ya “Konekt Umeme, Pika kwa Umeme” inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), katika viwanja vya Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Chalamila aliipongeza Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TANESCO pamoja na wadau wa maendeleo kwa kuanzisha programu hiyo ambayo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia umeme.
“Mpango huu ni mwanzo wa zama mpya katika sekta ya nishati nchini na unakwenda sambamba na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi na salama majumbani,” alisema Chalamila.
Kwa mujibu wa Chalamila, matumizi ya umeme kupikia si tu yanapunguza gharama bali pia ni njia salama, rafiki kwa mazingira na inayokuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Programu hiyo ya “Konekt Umeme, Pika kwa Umeme” inatajwa kuwa na gharama nafuu na kutumia kiwango kidogo cha umeme ukilinganisha na vyanzo vingine vya nishati kama mkaa na kuni, ambavyo vimekuwa vikichangia uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANESCO, Lazaro Twange, alieleza kuwa uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa nishati (Energy Compact), unaolenga kuwaunganishia umeme wateja milioni 8.5 ifikapo mwaka 2030. Hii ni sawa na kuwaunganisha wastani wa wateja milioni 1.7 kila mwaka.
Twange alibainisha kuwa kupitia mpango huu, mteja atapewa jiko la umeme wakati wa kuunganishiwa huduma hiyo na atalipa kidogo kidogo kupitia mfumo wa token, jambo ambalo litawawezesha wananchi wengi hasa wa kipato cha chini kupata fursa ya kupika kwa umeme.
Katika hatua ya kuhamasisha zaidi matumizi ya nishati safi, RC Chalamila aliwakabidhi wananchi mbalimbali majiko ya umeme na kuwataka kuwa mabalozi wa kampeni hiyo kwa jamii zao.
“Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha tunalinda mazingira na kuimarisha afya zetu kwa kutumia nishati safi ya kupikia. Hili ni jambo jema na la kuungwa mkono na kila Mtanzania,” alihitimisha Chalamila.