TANROADS NA MKANDARASI KUONDOA FOLENI MTO MZINGA

……………

Dar es Salaam, 09/10/2025

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na mkandarasi M/s STECOL Corporation ya China, kuanzia sasa watashirikiana kuyaondoa magari yatakayokuwa yameharibika kwenye barabara ya kuanzia eneo la Mbagala Rangitatu hadi Kongowe, ili kuepusha foleni za mara kwa mara.

Meneja wa TANROADS mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema kuharibika kwa mara kwa mara kwa magari makubwa eneo la mlimani na kutokana na wembemba wa barabara hiyo, na kutokuwa na mchepuko imekuwa ikisababisha foleni kubwa na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara hiyo kwa nyakati za asubuhi na jioni.

“Mkandarasi wetu anayejenga hii barabara ya njiasita kutokea Mbagala Rangitatu hadi hapa Kongowe kampuni ya M/s STECOL ya China tumekubaliana naye tutakuwa tunaondoa magari yote yatakayokuwa yakiharibika kwenye barabara hii, kwani ndio chanzo cha foleni kubwa na sio ujenzi unaoendelea sasa, na hii inafanyika hata kwenye barabara nyingine magari makubwa yakiharibika tunakwenda kuyatoa kwa kutumia mitambo au magari kuyavuta na kuyatoa eneo la barabara” amesema Mhandisi Kyamba.

Halikadhalika, Mha. Kyamba amesema pia TANROADS kwa kushirikiana na mkandarasi huyo watajenga njia za mchepuko kwa kiwango cha changarawe kwa upande wa kulia na kushoto mwa barabara kuu inayotumika sasa, ili kuruhusu magari mengi kupita bila ya kuwa na foleni.

Pia amesema kwa nyakati za asubuhi kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi saa 3:00 na kwa jioni kuanzia saa 11:00 hadi saa 2:00 usiku katika eneo la daraja la Mzinga kutakuwa na askari wa usalama barabarani watakaokuwa wakiongoza magari ili kuondoa kero ya foleni kwa madereva ambao wanachepuka na kuziba upande mmoja wa barabara.

Mha. Kyamba amesema serikali baada ya kuona wembamba wa barabara hii sasa inajenga njiasita kuanzia Mbagala Rangitatu hadi Kongowe yenye urefu wa Km 3.8, kwa lengo la kuepukana na changamoto ya foleni, na katika hizo njia mbili kila upande, na katikati barabara ya mabasi ya mwendokasi, pia kutakuwa na njia ya watembea kwa miguu na eneo la Kibada kutajengwa daraja la juu

Hatahivyo, ametoa wito kwa wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha ujenzi na pindi ujenzi utakapokamilika basi tatizo la foleni litakuwa historia.