Uamuzi wa Folz wawashtua mastaa Yanga, wabaki njiapanda

HUKO Yanga kila siku kuna jipya linaibuka. Si unafahamu hivi sasa Kocha Romain Folz yupo kwenye hatari ya kupoteza kibarua chake kama inavyoelezwa kutokana na presha iliyopo. Sasa kuna kitu amefanya.

Ipo hivi; wakati huu ambapo presha ya kupoteza ajira ya kuwa kocha mkuu wa Yanga ikizidi kwa Romain Folz, Mfaransa huyo amewashtua wachezaji wa timu hiyo na kuwaacha njia panda baada ya kubadilisha mambo.

FOL 01

Kuanzia Jumatatu wiki hii Oktoba 6, 2025, ambapo Folz amerejea kazini, amebadilisha programu nzima ya mazoezi ya timu hiyo ambayo imewaduwaza wachezaji wake.

Mastaa wa Yanga wanaeleza kwamba tangu ujio wa kocha huyo walikuwa hawapati muda mrefu wa kufanya mazoezi ya kuucheza mpira ndani ya ratiba ya mazoezi yao.

FOL 02

Mastaa hao wanasema kuwa kitu ambacho kilikuwa kinawachanganya kwa kocha huyo, alikuwa na ratiba ya kusimamisha mazoezi na kutoa sana maelekezo, hatua ambayo ilikuwa inapunguza muda wa mpira kupigwa.

“Tulikuwa hatuuchezei sana mpira, muda mrefu amekuwa akiutumia kutoa maelekezo, sasa hili wengi walikuwa hawavutiwi nalo hasa sisi wachezaji,” amesema kiungo mmoja wa kikosi hicho cha mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara.

FOL 03

Alichobadili Folz ni kwamba tangu timu hiyo irejee mazoezini Jumatatu Oktoba 6, 2025, walikutana na mazoezi ya mbio kwa siku mbili za kwanza lakini baada ya hapo wamekuwa wakiucheza mpira zaidi.

“Ni kweli amebadili, wengi tumeanza kufurahia mazoezi kwasasa, imetushtua sana, tunacheza sana mpira kuanzia Jumanne jioni mpaka jana (juzi), tunaucheza sana,” amesema nyota mwingine wa nafasi ya ushambuliaji.

“Mnaona ile picha alikuwa anacheka, kuna kitu alikuwa anafurahia kwenye hayo mazoezi ya kucheza na wote tukasema jamaa kacheka leo, alifurahia kitu.”

FOL 04

Yanga iko kwenye presha ya kumuondoa kocha huyo aliyeingoza timu hiyo katika mechi tano za mashindano kisha akashinda nne na sare moja. Hajapoteza.

Mashabiki wa Yanga na hata baadhi ya viongozi wake hawakubaliani na Folz na namna kikosi hicho kinacheza, wakijipanga kufanya mabadiliko kwenye benchi hilo la ufundi.

Jina la Romuald Rakotondrabe ‘Roro’ ambaye ni kocha aliyeiongoza Madagascar kumaliza katika nafasi ya pili kwenye michuano ya CHAN 2024, linatajwa kurithi mikoba ya Folz endapo ataondoka.

Taarifa zinabainisha kwamba, Roro na Yanga wamekubaliana kila kitu, kilichobaki ni kocha huyo kuja nchini, kisha Yanga kutangaza kuachana na Folz ili aanze kazi rasmi.

Yanga kwa sasa inajiandaa na mechi ya hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi ikianzia ugenini Oktoba 18, 2025.