Wakulima wa tumbaku kulipwa fedha zao kabla ya Oktoba 30

Tabora. Kampuni za ununuzi wa tumbaku nchini zilizo chelewesha malipo ya wakulima kwa msimu wa kilimo uliopita, zimetakiwa kuhakikisha zinalipa madeni hayo kabla ya Oktoba 30, mwaka huu.

Wakulima hao wanadai zaidi ya Sh5 bilioni, ambazo ni malipo ya tumbaku ya msimu wa kilimo uliopita.

Kampuni husika zimeelekezwa kulipa madeni hayo pamoja na riba, ikiwa ni fidia kwa ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.

Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi Oktoba 9,2025 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa kikao cha waziri huyo na viongozi wa vyama vya ushirika, benki na kampuni za ununuzi wa tumbaku kilichofanyika Kata ya Chemchem manispaa ya Tabora.

Wakuu wa wilaya za Tabora Upendo Wella(Kushoto)na mkuu wa wilaya ya Sikonge Thomas Myinga wakisikiliza maelekezo ya waziri wa kilimo katika kikao chake na wadau wa Tumbaku kilichofanyika Chem chem manispaa ya Tabora.Picha na Hawa Kimwaga

“Nawapa siku hizi 21 yaani mpaka kufikia terehe 30 nisisikie habari ya mkulima ambaye hajalipwa fedha zake tafadhali sana tusichokozane kabisa, haiwezekani mpaka msimu mwingine unataka kuanza mkulima bado anadai fedha za msimu uliopita,” ameagiza Bashe.

Amesema kampuni hizo kwanza zikaandike maelezo polisi ya kwa nini hawajalipa wakulima mpaka muda huu, lakini pia wakathibitishe kila mmoja kwenye eneo lake kuwa atalipa lini na iwe ni kabla ya tarehe 30 mwezi huu.

“Kaandikeni maelezo kituo cha polisi kwa nini wakulima hawana fedha zao mpaka sasa wakati tumbaku yao mmechukua mapema sana,” amesema.

Kuhusu mpango wa kuwasajili wakulima, kampuni za ununuzi wa tumbaku, taasisi za fedha kwa kushirikiana na Serikali zimetakiwa kuwasajili wakulima katika mfumo rasmi ambao utakua na taarifa muhimu za mkulima ikiwemo ukubwa wa shamba alilolima, mazao aliyolima hivyo asomeke kwenye mfumo nchi nzima.

Wadau wa Tumbaku wakisikiliza maelekezo ya viongozi juu ya maboresho ya maslahi ya wakulima.Picha na Hawa Kimwaga

“Wakulima wakisajiliwa mmoja mmoja ndani ya vyama vyao itatusaidia kudhibiti wizi na utoroshaji wa tumbaku na hata tabia ya uchakachuaji wa tumbaku, hiyo kwani kila mmoja atabainika amelima kiasi gani na amevuna kiasi gani na itasaidia pia mkulima akipata changamoto aweze kupata fidia,” ameongeza Bashe.

Hata hivyo, ametoa angalizo kwa kampuni ambayo haitashiriki kuwezesha zoezi la usajili wa wakulima wa Tumbaku basi haitopata kibali cha kununua Tumbaku msimu ujao wa Kilimo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ameweka mkazo suala la kampuni zinazodaiwa kuripoti polisi kila mara mpaka hapo watakapomaliza malipo ya wakulima.

Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Matiko Chacha akizungumza katika kikao cha waziri wa Kilimo na wadau wa Tumbaku nchini kilichofanyika katika kata ya Chem chem manispaa ya Tabora.Picha na Hawa Kimwaga

“Wanapaswa waje hapa mpaka hapo watakapowalipa wakulima fedha zao, kwanza wanatusumbua sana na huu si wakati wakuanza kusumbua malipo ya wakulima,” amesema Chacha.

Miongoni mwa maazimio ya kikao hicho ni kwamba wakulima pia wajiunge na bima ili kuwasaidia pale watakapopata majanga iwe rahisi kufidiwa hasara hiyo huku ikisisitizwa kuwa bei ya ununuzi wa tumbaku haitopungua na hii ni kutilia mkazo lengo la kumnufaisha mkulima wa zao hilo.

Onesmo Ngonyani mkulima wa tumbaku akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzie amesema usajili kwao ni bora kwa sababu itawasaidia wale wanaolangua tumbaku kwa njia zisizo sahihi na kuwatia hasara.

“Kama hivi mtu analangua tumbaku zetu bei chini anawahi anajaza ‘magodauni’ kwa sababu ana mtaji mkubwa sisi tunabaki kusubiri, lakini mwingine anatorosha inabidi tumlipie,” amesema Onesmo.