Wananchi waonywa kutoingizwa kwenye siasa za uchochezi kuelekea uchaguzi mkuu

Moshi. Wananchi wametakiwa kuepuka kutumika kwa malengo ya kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Badala yake, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika hatua hiyo muhimu ya kikatiba kwa amani, utulivu, na mshikamano.

Wito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, Yuvenal Shirima, wakati akiwapokea vijana 14 kutoka mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar, waliopanda Mlima Kilimanjaro kwa muda wa siku nne kwa lengo la kuhamasisha amani na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza katika hafla ya mapokezi iliyofanyika katika lango la Marangu, linalotumika kwa ajili ya kupandia Mlima Kilimanjaro, Shirima amesema kuwa uchaguzi ni haki ya kikatiba inayopaswa kutekelezwa kila baada ya miaka mitano.

Hivyo basi, amewataka Watanzania kupuuza upotoshaji wa kwamba siku hiyo ni ya maandamano, na badala yake kuitumia kushiriki kwa amani katika mchakato wa kidemokrasia.

“Oktoba 29, 2025 ni siku ya uchaguzi mkuu. Uchaguzi siyo wa chama fulani, ni wa kitaifa na ni takwa la kikatiba. Kila Mtanzania ana wajibu wa kwenda kupiga kura kuwachagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo,” amesema Shirima.

Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuimarisha ulinzi na usalama katika kipindi cha kampeni na siku ya uchaguzi, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kupiga kura bila hofu.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vijana Nguvu Kazi Kizimkazi Zanzibar, Abusufiani Yakuti Juma, ambaye aliongoza msafara wa vijana hao, amesema walipandisha bendera ya Taifa yenye picha ya mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni ishara ya kuhamasisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

“Tumejifunza kuwa uimara wa taifa unajengwa na vijana. Hatutaki kuyumbishwa, tunasubiri siku ya uchaguzi ili tutimize wajibu wetu wa kikatiba wa kupiga kura,” amesema Juma.

Vijana waliopanda mlima kilimanjaro wakikabidhi bendera kwa mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Moshi vijijini Yuvenal Shirima baada ya kushuka

Amesema safari hiyo pia imelenga kuhamasisha vijana kushiriki katika shughuli za utalii wa ndani na kuutangaza Mlima Kilimanjaro kama urithi wa taifa na kivutio cha kimataifa.

Kassim Mandwanga, kijana kutoka Morogoro, amesema walipandisha bendera hiyo kumpongeza mgombea urais wa CCM, kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Watanzania.

Haidari Yahaya Issa kutoka Zanzibar amesisitiza kuwa changamoto ya kupanda mlima imewafundisha uzalendo, uvumilivu na mshikamano.

Vijana hao 14 kutoka mikoa 10 ya Tanzania Bara na Zanzibar walianza safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia lango la Marangu Oktoba 4, mwaka huu.