Bunda. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira ametoa tahadhari kwa wananchi kuhusu kikundi cha watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kusambaza chokochoko, akisema hawawezi kuisumbua nchi wala kufanikisha dhamira zao ovu.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 9, 2025 kwenye mkutano wa kampeni za urais uliohutubiwa na mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan mjini Bunda, Wasira amesema amani na utulivu vitaendelea kutawala nchini licha ya upotoshaji unaofanywa mtandaoni.
“Zipo chokochoko nyingi, lakini si za wananchi wengi, ni za wachache mitandaoni. Naomba msome kwa makini. Wapo watu wasiotoridhika, hata ukifanya vizuri namna gani wao wananuna, ndivyo walivyo,” amesema.
Akimnukuu kwa mfano wa maharage machache yasiyoiva, Wasira amesema watu hao hawawezi kuathiri mustakabali wa nchi, huku akimwambia Samia asibabaishwe na maneno yao.
Wasira ameeleza kuwa CCM imewaletea wananchi mgombea urais mwenye mafanikio makubwa, ambaye ameonyesha uwezo wa utekelezaji wa ilani ya chama.
“Hatuwaletei mgombea ‘lena’, tunawaletea rais aliyefanya kazi kubwa kwa mafanikio makubwa,” amesisitiza Wasira.
Amefafanua kuwa Samia alikabiliwa na changamoto kubwa alipoingia madarakani, ikiwamo ya mlipuko wa Kovid-19, kifo cha aliyekuwa Rais, John Magufuli na kuporomoka kwa uchumi.
“Alitumia kauli mbiu ya ‘Kazi Iendelee’, miradi mikubwa kama reli ya kisasa imeendelea hadi Makutupora, na Bwawa la Nyerere sasa limekamilika kwa zaidi ya asilimia 70,” amesema.
Katika sekta ya elimu na afya, Wasira amesema Bunda pekee zimejengwa shule mpya 13 za msingi, shule 15 za sekondari, zahanati 20, vituo vitatu vya afya na hospitali moja.
Aidha, amesema hatua hiyo ya Samia imepunguza vifo vya wajawazito kutoka 500 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia 100.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Pangani, Jumaa Aweso amesifu jitihada za Samia kwenye sekta ya maji, akisema miradi yenye thamani ya zaidi ya Sh20 bilioni imetekelezwa Bunda, ikiwamo mradi wa Nyabeho uliogharimu Sh10 bilioni.
“Hali ya upatikanaji maji Bunda imeboreshwa kwa zaidi ya asilimia 87 kwa wakazi wa mjini, na vijijini nako miradi inaendelea. Zaidi ya Sh bilioni 100 zimetolewa kusukuma maji kutoka Ziwa Victoria hadi Bunda na Tarime,” amesema.