Wataalamu wahimiza uwekezaji wa elimu bora na ubia kujenga uchumi jumuishi

Iringa. Wadau wa maendeleo na wataalamu wa uchumi wameitaka Serikali, taasisi za elimu, na sekta binafsi kuongeza ushirikiano katika uwekezaji wa elimu bora na ubia endelevu, ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi jumuishi kwa Watanzania wote.

‎Hayo yamesemwa leo Alhamisi Oktoba 9, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha (Rucu), Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, wakati wa kongamano la kitaaluma lenye kauli mbiu “Je, tunajenga uchumi jumuishi?” lililoandaliwa na Rucu kwa kushirikiana na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC).

‎Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Katoliki Ruaha, Profesa Chrispina Lekule amesema chuo hicho kinatambua umuhimu wa Serikali kuunganisha sekta binafsi na taasisi mbalimbali ili kuweka ushirikiano wa kimkakati katika uchumi wa Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, akiwasilisha mada ya“Hali ya uwekezaji, dhana ya ubia na nafasi ya ubia katika ujenzi wa uchumi jumuishi,” katika ukumbi wa mikutano uliopo Chuo kikuu Katoliki Ruaha kilichopo halmashauri ya Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias


‎Akiwasilisha mada yenye kichwa “Dira 2050 na nafasi ya elimu bora kwa maendeleo ya rasilimali watu,” Profesa Lekule alisema elimu bora ndiyo chombo muhimu cha kujenga uchumi, kwani inamjenga mtu kuwa mbunifu, mwenye maadili na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.

‎Amesema kuwa taasisi za elimu zinapaswa kuongeza tafiti zinazolenga kutatua changamoto za wananchi badala ya kujikita tu kwenye nadharia na kwa kufanya hivyo, vyuo vitakuwa sehemu ya suluhisho la matatizo ya kijamii na kiuchumi.

‎“Mfumo wa elimu hauzalishi wahitimu pekee, bali viongozi na wasomi wenye uwezo wa kuleta mabadiliko katika jamii,” amesema Profesa Lekule.

‎Amebainisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inalenga kujenga uchumi jumuishi unaowagusa wananchi wote, hivyo elimu bora ni msingi wa kufanikisha hilo.

‎“Kila Mtanzania anapaswa kujiuliza anachangiaje kuboresha elimu na maendeleo ya Taifa badala ya kulalamika tu,” ameongeza.

‎Aidha, Profesa Lekule amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kiuchumi, lakini bado kuna changamoto ya ujuzi usiokidhi mahitaji ya soko na upungufu wa ajira hasa kwa vijana na wanawake na kuwa mabadiliko ya mitaala yanapaswa kuzingatia ubunifu na ujuzi wa karne ya 21, kukuza motisha kwa walimu, na kuongeza tafiti vyuoni.

‎Pia Profesa Lekule ameitaka Serikali kuendelea kuimarisha uwekezaji katika elimu na sekta za kimkakati ili kukuza uchumi wa Taifa.

‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, akiwasilisha mada ya “Hali ya uwekezaji, dhana ya ubia na nafasi ya ubia katika ujenzi wa uchumi jumuishi,” amesema uchumi wa Tanzania unategemea ubora wa watu wake na kwamba rasilimali watu ni nguzo kuu ya maendeleo.

‎“Nchi yoyote duniani uchumi wake unaamuliwa na ubora wa watu wake,” amesema Kafulila, akiongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha changamoto ya ajira kwa wahitimu inatatuliwa kupitia programu za ubia kati ya sekta binafsi na umma.

‎Kafulila amesema vichocheo vya uchumi wa Tanzania vinahusisha jiografia ya nchi, sekta ya madini, utalii, ardhi na kilimo cha umwagiliaji ambacho kinatoa ajira na chakula cha uhakika.

‎Amesema sekta ya madini na diplomasia ya uchumi zimechangia kupanda kwa mapato ya nchi kutoka dola milioni 17 mwaka 2021 hadi dola milioni 32 mwaka 2024.

‎ ‎Mwandishi wa habari nguli na mwongozaji wa kongamano hilo, Tido Mhando, amesema majadiliano hayo ni sehemu ya mwelekeo wa kitaifa kuelekea uchumi shindani na jumuishi, unaohusisha wadau wote.

‎Mchokoza mada, Profesa Samwel Wangwe, amezungumzia  maeneo ya kimkakati ya kiuchumi yanayoweza kufanikishwa kwa ubia, akibainisha kuwa dira ya maendeleo inapaswa kuwekewa msingi wa vitendo ili matokeo yake yaonekane.


‎Kwa upande wake Profesa Humphrey Mushi, akijibu swali kuhusu nafasi ya vijana katika dira hiyo, alisema ni lazima nchi ijue inapokwenda na kuweka vipaumbele vinavyoendana na uhalisia wa soko la ajira.

‎“Toka awamu ya tano, Tanzania imejikita katika viwanda na ina misingi imara ya kufikia uchumi jumuishi kutokana na uwepo wa rasilimali watu, uongozi thabiti, na huduma bora za kijamii,” alisema Profesa. Mushi.

‎Wakati wa majadiliano, washiriki kadhaa waliuliza namna PPPC itakavyowahusisha wananchi kuelewa dhana ya uchumi jumuishi na dira ya maendeleo 2050.

‎Dk Anne Malipula kutoka RUCU aliuliza, “Je, mnahakikisha vipi kuwa wananchi wote wanafahamu kuhusu uchumi jumuishi kuelekea 2050?”


‎Akijibu swali hilo, Profesa Wangwe alisema tayari kuna miezi tisa ya maandalizi kabla ya kuanza utekelezaji rasmi wa dira hiyo, ambapo wananchi watashirikishwa kikamilifu.
‎ ‎
‎Akifunga kongamano hilo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya barabara ili kuwezesha uzalishaji kuendelea katika maeneo mbalimbali na kurahisisha watu kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa juhudi pia zinaelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwa lengo la kuwawezesha wakulima wa Iringa kuzalisha kwa tija na kuinua uchumi wa wananchi.

‎Aidha, amesema Serikali inaendelea kukuza sekta ya utalii mkoani humo ili kuongeza mapato na fursa za ajira kwa wananchi, hivyo ni muhimu kwa kila mwananchi kufahamu nafasi yake katika kufanikisha uchumi jumuishi kama sehemu ya utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa ya 2050 huku akiwataka wananchi kutumia elimu waliyonayo kuchochea maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla.

‎Kuhusu mmomonyoko wa maadili, Mkuu huyo wa Mkoa wa Iringa amebainisha kuwa ni tatizo linaloikumba jamii kwa ujumla na si vijana peke yao, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika katika kulikabili tatizo hilo ili kulinda misingi ya malezi, maadili na maendelezo ya kizazi kijacho.

‎Ikumbukwe kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ilizinduliwa Julai 17, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma na dira hiyo itaanza kutekelezwa rasmi mwaka wa fedha 2026/2027, ikilenga kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki moja kwa moja katika uzalishaji, matumizi ya rasilimali, elimu, afya, teknolojia na fursa nyingine zinazoinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.