Dereva wa kampuni ya ujenzi afariki dunia gari ikipinduka, konda wake ajeruhiwa

Pemba. Dereva wa gari la kubebe na kuchanganya zege la kampuni ya IRIS inayotengeneza barabara Pemba, Nassor Fatawi Iddi (25) mkazi wa Machomanne amefariki dunia huku Msaidizi wake Atanas Joseph akinusurika baada ya gari lao kupinduka Mkoa wa Kusini Pemba.

Ajali hiyo imetokea mita 15 baada ya kuvuka daraja upande wa Chakechake Kusini Pemba.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kaskazini, Mussa Mwakasula leo Oktoba 10, 2025 amethibisha kutokea ajali hiyo ambapo gari aina kampuni ya IRS imepinduka na dereva kufariki hapo hapo.

Kwa mujibu wa mashuhuda kuhusu ajali hiyo wamesema walifika katika eneo la ajali walilikuta gari hilo likiwa limelala baada ya kugonga ukuta wa Mlima wa Chamanangwe na dereva akiwa ameshafariki na majeruhi kupelekwa Hospitali ya Wilaya Kinyasini Wete.

Said Hamad Ali amesema baada ya kufika eneo la tukio aliona dereva akiwa katika siti yake ya mbele ikiwa kwenye hali mbaya kwa kubanwa.

Amesema tukio hilo limewasikitisha sana kuona kijana yupo kwenye hali ngumu na huku wasamaria wema wakijitokeza katika kumsaidia kijana huyo lakini hata baada ya kutolewa tayari alishaiyaga dunia.

‘’Nimeshuhudia tukio hili nilipokuja nikamuona dareva akiwa katika siti yake ya mbele akiwa amebanwa na kule mbele akiwa katika hali ngumu,’’amesema Said.

Mwananchi Mwingine ni Hamad Mussa Ali mkazi wa Kambini Kichokochwe amesema baada ya kufika eneo hilo alisikia kuwa gari hiyo ilikuwa na inawatu wa wili akiwa dereva na konda wake.

‘’Mimi nilipofika sikuona ajali ilivyokuwa ila niliona mwili ukiingizwa kwenye gari la wagonjwa,” amesema.

Daktari katika Hospitali ya Kinyasini, Bedui Nassor Mbarouk amesema ameupokea  mwili wa marehemu ukiwa na  majeraha ya nje na ndani ya mwili  jambo ambalo limesababisha kifo chake.

Amesema baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu alibaini aliumia maeneo ya kichwani na kifua kwa kubanwa maeneo ya mbele na ndio sababu ya kifo chake.

Kaimu daktari dhamana wa Hospitali ya Micheweni, Rashid Daud Mkasha ambaye amempokea majeruhi wa ajali hiyo saa 2:00 asubuhi Joseph Atanas amesema baada ya kumfanyia uchunguzi amepelekwa Hospitali ya Mkoani kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.

‘’Tumepokea kijana huyo majira ya saambili asubuhi na katika uchuguzi wao tulibaini kukatika kwa mfupa na kumsafirisha kumpeleka Hospitali ya Rufaa Mkoani ambako ndio kwenye wataalamu wa maswala ya mifupa’’amesema Mkasha