Dar es Salaam. Wengi wakisikia mgonjwa yupo hospitali kitengo cha uangalizi maalumu (ICU) kinachokuja akilini haraka ni kuumwa moyo au amepata ajali. Wachache wanajua kuwa ndani ya hospitali huwa kuna wagonjwa mahututi wa afya ya akili.
Humo, maisha ya binadamu yanapimwa si kwa mapigo ya moyo pekee, bali kwa utulivu wa nafsi na nguvu ya akili.
Joakhina Mazengo ambaye amehudumu katika kitengo hicho Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa zaidi ya miaka 10, amekuwa sehemu ya maisha ya wagonjwa hao, wale wanaopambana si na maradhi ya mwili pekee, bali na mawimbi makali ya akili.
Na dunia inapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Afya ya Akili Oktoba 10, 2025, tumekusogeza msomaji mpaka katika ICU hii, ili uelimike na kuijali afya yako ya akili, wewe pamoja na wanaokuzunguka.
“Nilijua siwezi kubaki hapa,” Joakhina anakumbuka siku yake ya kwanza mwaka 2015 alipohamishwa kitengo na kupelekwa katika wodi hiyo.
“Nilivyoingia tu, nilihisi siwezi kufanya kazi hapa,” anasema kwa tabasamu hafifu.
“Wagonjwa walikuwa wanapambana, wengine wanaingizwa wodini kwa nguvu, wengine wanapiga kelele. Nilihisi ni kazi isiyowezekana.”
Anasema alitumia siku chache za mwanzo kama mtazamaji wa kimya, akiangalia wauguzi wazoefu wakidhibiti wagonjwa kwa ustadi na upole mkubwa.
“Nilivyokaakaa pale nikawa naangalia niliowakuta wanawadhibiti vipi wagonjwa, kwa kuwa sisi ni wageni, hasa kwa mwanamke, wale wagonjwa huwawezi, wana nguvu. Nikawa naona wafanyakazi wengine wa kiume wanapambana kuwakamata, mimi naambiwa niandae dawa za sindano, napeleka pale wanampa mgonjwa anatulia. Nilikuwa siwezi kwenda kuona mgonjwa, nikaenda mbele pale, naogopa nitatolewa meno,” anasimulia na kucheka.

Anasema kuna nyakati alishangaa, madaktari aliowakuta, wauguzi na wahudumu wanadhibiti vipi mtu mwenye nguvu mara tatu ya mtu wa kawaida? Lakini baadaye, alijifunza kwa macho na moyo.
“Kwa sasa nimeshajua mgonjwa anapokuja, nikae vipi ili apitishwe wodini, mpaka sasa nimezoea akija mgonjwa anaumwa sana nami najua nitakaa namna gani, basi nakuwa sawa na salama.”
Hata hivyo, Joakhina anasema kufanya kazi katika kitengo hicho kunahitaji moyo, kwani watumishi kwa ujumla hukumbana na changamoto kadhaa, ambazo kwa upande wake anasema awali zilimpa wakati mgumu, lakini kwa sasa anaziona kama ni sehemu ya kazi yake.
“Tushapigwa ngumi mle, wale tunawachukulia ni wagonjwa, wengine wanatukana, anaweza akakutukana mno, sasa nyakati hizo unaumia na mwingine nikimwangalia ni mwanangu, namzaa lakini ni mgonjwa, tunavumilia.
“Tunajua ni wagonjwa, si kwa makusudi. Baadaye wakipata nafuu, unamwambia ulifanya hivi na vile wanakuomba msamaha, ‘mama nisamehe, sikudhamiria.’”
Kufanya kazi katika kitengo hicho si hatari pekee, anasema ni muhimu mfanyakazi awe na moyo wa uvumilivu, kwani kuwepo kila siku katika kitengo hicho ni somo jipya.
Joakhina anasema kuna changamoto kadhaa zinazowakabili, akitaja mojawapo ni idadi yao ndogo ilhali wagonjwa wana nguvu, na wakati mwingine wafanyakazi wachache wanakabiliana na changamoto kubwa ya usalama.
“Wagonjwa hawa wanapokuja huwa na nguvu, inabidi tuwe watu wengi kuwadhibiti. Wakati mwingine, ukiona amezidi nguvu, lazima uache mlango wazi, maana ni hatari,” Joakhina anasema.
Anapendekeza Serikali iongeze idadi ya watumishi katika ICU hiyo maalumu, ambayo Mwananchi ilishuhudia vitanda vikiwa vimejaa wagonjwa waliofungwa kwa kamba miguu na mikono yao.

Kwa Joakhina, tiba ya wagonjwa wa akili haipaswi kuishia hospitalini. Anaamini tiba endelevu inapaswa kuhusisha maisha ya mgonjwa hata baada ya kupona.
“Wagonjwa wengine wanapona vizuri hapa, lakini wakirudi nyumbani wanakosa msaada. Wanaanza tena kutumia bangi au pombe na baada ya muda wanarudi hospitali.”
Anashauri; “Serikali ingeanzisha kituo cha kazi za mikono kwa wagonjwa waliopona. Wapewe mashamba, au shughuli za kufanya ili wabaki kwenye mfumo mzuri wa maisha. Kazi inaweza kuwa sehemu ya tiba.”
Joakhina, mwenye miaka 35 tangu aanze kazi kama mhudumu wa afya, anaona kazi hiyo kama wito unaomhitaji mtu awe na huruma ya kweli.
“Hawa wagonjwa wanahitaji mtu wa kuwajali. Si wagonjwa wa akili pekee, ni wagonjwa kama wengine. Unapowaona wakipona na kurudi nyumbani, moyo unajisikia fahari, unajua umegusa maisha.”
Kwa miaka yote aliyofanya kazi hiyo, Joakhina anaamini kuwa mafanikio makubwa zaidi si tu kuona mgonjwa akipona, bali kuona jamii ikibadilisha mtazamo wake.
“Natamani siku moja jamii itambue kuwa wagonjwa wa akili wanastahili heshima na upendo kama wengine. Wapate nafasi ya pili maishani,” ameeleza matamanio yake.
Joakhina licha ya majukumu yake mengine anayopaswa kufanya ikiwemo kuandaa dawa, Mwananchi ilishuhudia akifua moja ya kamba nyeupe, inayotumika kuwafunga wagonjwa waliopo ICU, huku akipiga soga na mmoja wa wagonjwa aliyepo ndani ya wodi hiyo.
Pamoja na hayo, Joakhina anaendelea kufanya kazi kwa moyo uleule aliouanza nao miaka 10 iliyopita, akitunza, akituliza na kurejesha utu wa wale wanaopotea kwenye giza la akili.