:::::::
Jeshi la Polisi nchini Tanzania kupitia msemaji wake DCP David Misime limesisitiza kuhusu matumizi sahihi ya mitandao ya Kijamii pamoja na ulinzi wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa Tanzania, akibainisha kuwa Jeshi hilo limejipanga kikamilifu kushughulika kikamilifu na wote watakaohatarisha amani ya nchi.
Msemaji huyo pia ameonya kuhusu wanaotumia mitandao vibaya kuhamasisha chuki, uhasama na kusambaza taarifa za kuzusha, akisema sheria inatoa adhabu pia kwa mtumiaji wa mitandao ya kijamii atakayesambaza (kushare) taarifa ambazo hazina ukweli ama ambazo zine lengo la kuzua taharuki na uhasama.
“Mitandao ya kijamii tukiitumia vibaya inaweza kutufikisha pabaya ikiwemo kutumika kama silaha kuleta uhasama, uzushi na kusambaza uongo kama ambao tunauona kwenye mitandao na nitoe wito kwa jamii unaposambaza taarifa ambazo sio sahihi ni kosa pia kwako unayesambaza taarifa potofu.” Amesema Kamanda Misime.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari leo Oktoba 10, 2025, Misiime pia ameeleza kuwa wamejipanga vyema kulinda raia na mali zao siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi Mkuu, akiwapongeza watanzania kwa kuendelea kuelimika na kukuza ustaarabu wao wakati wote wa kampeni, akiomba ushirikiano zaidi wa kufichua uhalifu na wahalifu kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Tanzania.
Amewatoa hofu pia Watanzania kuhusu yanayoendelea mitandaoni, akisema nchi ni salama na hakuna tatizo lenye kutishia usalama na utulivu siku ya upigaji wa kura, akisema Jeshi la polisi linaendelea kuchukua hatua kwa wanaotumia mitandao hiyo vibaya na kuishukuru serikali kwa uwezeshaji wake mkubwa wa vifaa na vitendea kazi katika udhibiti wa uhalifu na wahalifu.
Amesema Jeshi hilo pia limesambaza Askari polisi zaidi ya 3,900 kwenye Kata zote za Tanzania bara pamoja na Askari 388 kwenye Shehia za Zanzibar wakitoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya mitandao na kuwataka wazazi kuelimisha pia Vijana wao dhidi ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuheshimu sheria za Tanzania.