WANANCHI WA CHATO KUSINI MJIANDAE KULA BATA

Mgombea wa Ubunge Jimbo la Chato Kusini,Paschal Lutandula, akiomba kura kwa wananchi

…………..

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chato kusini(CCM) Paschal Lutandula, amewaahidi wananchi kujiandaa kula Bata iwapo watamchagua kuwa Mbunge katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2025.

Amesema hakuna sababu ya wananchi kuendelea kulialia kila mwaka, na kwamba amejipanga kuinua uchumi wa Jimbo hilo ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, kwa madai kuwa kila mwananchi atanufaika na maendeleo yatakayo patikana jimboni humo.

“Mimi sitokuwa Mbunge wa maneno mengi ispokuwa vitendo, nataka wananchi katika kipindi changu cha miaka mitano muinue uchumi wenu kisha mle Bata”,

“Ndiyo maana kauli mbiu yangu ni baada ya kazi tunakula Bata, Jimbo hili nataka lipae kwa maendeleo na niwasihi waliokuwa na mpango wa kuhama watukizane kwa sababu maendeleo ya kweli sasa yanakwemda kuonekana kwa kipindi kifupi sana”,

“Ninayo dhamira ya kweli ya kuwatumikia Baba na mama zangu,maana mimi ni mtoto wenu siwezi kuja hapa kuwadanganya, naomba mniamini mimi,mgombea Urais kupitia CCM, mama yetu Samia Suluhu Hassan I pamoja na mgombea wetu wa Udiwani kwenye Kata hii ya Nyarutembo.

Ameahidi hayo akiwa kwenye Kijiji cha Nyarutembo, Kata ya Nyarutembo wilayani humo mkoani Geita wakati wa mkutano wa kampeni huku akiahidi kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa kwenye shule ya msingi Nyarutembo ambayo haijawahi kuongezewa hata chumba kimoja tangu mwaka 2017.

Aidha anakusudia kuongeza idadi ya visima virefu na vifupi kwenye kata hiyo ili kupunguza adha ya kugombea maji kwenye kisima kimoja kilichopo kwa sasa.

Vilevile amewasisitiza wananchi kuendelea kuzaliana kwa sababu ya mipango mizuri ya afya iliyoandaliwa na serikali kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ambayo inaeleza kuwa wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kutibiwa bure.