MSHAMBULIAJI wa TRA United, Adam Adam amemzungumzia kiungo wa Yanga, Maxi Nzengeli namna alivyo hatari kutokana na kupatikana maeneo mengi ya uwanja wakati wa mechi, akiamini hilo linamtofautisha na wengine na kusisitiza ataisaidia timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Adam alisema Nzengeli katika mechi moja anaweza kuonekana winga ya kulia, kushoto na namba 10, jambo linalomsaidia kufunga mabao na kuwapa wachezaji wenzake pasi za mwisho (asisti).
Msimu wa 2023-2024, Maxi alicheza dakika 2090, akifunga mabao 11 na kutoa asisti mbili, huku akicheza mechi 23. Pia msimu wa 2024-2025 alifunga mabao sita na asisti 10. Tayari msimu huu 2025-2026 ana bao moja, jambo ambalo Adam amemtaja kama ni hatari zaidi uwanjani.
“Mechi ya kirafiki tuliyocheza na Yanga Ijumaa kwenye Uwanja wa Gymkhana ambayo tulitoka suluhu, Nzengeli alifanya kazi kubwa ya kupatikana kila eneo, hilo linaifinya timu pinzani kwa kuweka umakini wa kumkaba,” alisema Adam na kuongeza;
“Katika mechi za kimataifa naamini akiendelea kufanya hivyo, itawapa mwanya wachezaji wengine wa Yanga kutumia upenyo huo kufunga wakati wapinzani wakimkaba Nzengeli.
“Kuhusu mechi ya kirafiki tuliyocheza na Yanga ilikuwa kipimo kizuri, kutokana na ubora wa kikosi cha klabu hiyo, tulicheza kwa nidhamu ikatusaidia kumenteini mchezo.”
Maxi alitua Yanga Julai 2023 akitokea Maniema ya kwao DR Congo. Tangu atue kikosini hapo, amekuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha timu hiyo akiisaidia kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2023-2024.