Hekaya za Mlevi: Unawajua Wazungu Weusi? 

Dar es Salaam. Mwezi huu tunatimiza miaka ishirini na sita toka kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Leo nimeona niilete kwenu sehemu ya hotuba aliyoitoa mwaka 1962 wakati anaunda Wizara ya Sanaa ya Taifa na Vijana. 

Ni miaka  sitini na tatu toka Mwalimu alipotoa  hotuba hii, Je, ndoto yake ilitimizwa na inaendelezwa? Mwalimu alisema hivi,  “….Badiliko kubwa nililofanya ni kuunda wizara mpya, Wizara ya Sanaa ya Taifa na Vijana. 

Nimefanya hivyo kwa sababu naamini kuwa mambo ya sanaa ndio roho ya maisha ya taifa lolote. Nchi isiyo na sanaa yake ya asili ni mkusanyiko wa watu tu ambao hauna roho. 

Katika madhambi yote yaliyofanywa na ukoloni, hakuna dhambi kubwa zaidi kuzidi jitihada iliyofanywa kutufanya tuamini kuwa hatukuwa na mambo yetu ya sanaa ya kiasili, au kwamba kama yalikuwako yalikuwa ni mambo ya kishenzi yanayofaa kutufanya tuone haya, sio ya kutufanya tuone fahari.

Baadhi yetu hasa wake tuliopata elimu ya Kizungu, tulifanya jitihada kubwa sana, kuwaonyesha watawala wetu wa kikoloni kwamba tumestaarabika.  Na kustaarabika maana yake ilikuwa ni kuacha mambo yote ya asili yetu na kuiga mambo ya kizungu.

Jitihada kubwa ya vijana wetu hata hivi leo, sio jitihada ya kuwa Waafrika wenye elimu ya kisasa, bali ni jitihada ya kuwa wazungu weusi. Kwa kweli wakati mmoja ilikuwa ni sifa sio tusi kumwita Mwafrika anayeiga uzungu, Mzungu Mweusi. 

Tulipokuwa shuleni tulifundishwa nyimbo za kizungu, wangapi tulifundishwa nyimbo za Kinyamwezi na Kihehe? Wengi wetu tunaweza kucheza ngoma ziitwazo rumba, cha cha cha , rock n roll na hata waltz sijui  na foxtrot na mengineo, ni wangapi kati yetu ambao tunaweza kucheza au tulipata kusikia kuwa kuna ngoma iitwayo Gombesugu, mangala, kongo, nyang’ulu, kiduo, lelemama na mengineo. 

Waafrika wangapi, hasa waliosoma wanaweza kupiga zile ngoma zilikuwa zikipigwa jana? Wangapi wanaweza kucheza nanga au zeze au marimba au  kilanzi au ligombo au mangala? Na ingawa twacheza dansi na kucheza mapiano, tukitaka kusema kweli ni mara ngapi ambapo dansi,  japo ni rock au twist inaweza kutuchemsha damu kama tunavyochemshwa na mganda au gombesugu. 

Tunavyoweza kuchemshwa na mganda au gombesugu japo vyombo vyake ni kokoto tu katika makopo. Ni vigumu damu ya binadamu kuchemka na mwili wake ukasisimka kwa ngoma na nyimbo ambazo sio za asili yake.

Nimeanzisha wizara hii ili isaidie kufufua fahari yetu katika mambo yetu ya asili, ningependa tutafute mambo yetu yote yanayofaa kutoka katika kila kabila bila kuacha hata kabila moja au jambo moja na yafanywe mambo hayo kuwa ni mambo ya taifa zima la Tanganyika. Natumaini kuwa kila mmoja wetu atasaidia wizara mpya hii. 

Lakini sitaki mtu afikiri kuwa kufufua mambo yetu maana yake kupuuza mambo ya kigeni, nchi ambayo haikubali kuiga mambo ya kigeni ni nchi ya wapumbavu na wenda wazimu. 
Maendeleo ya binadamu yasingewezekana kama tusipokubali kuiga, lakini kuiga sio maana yake kuacha mambo ya asili yetu. Kuiga kwa maana ni kule kunakosaidia kuyafanya mambo ya asili yetu yapendeze zaidi…”

Wakati wa enzi ya uongozi wake na hata miaka kadhaa baada ya kung’atuka kwake  mambo mengi aliyoyategemea yalikuwa yakiendelea.  Sanaa zetu za asili zilitawala kila kona. Kulikuwa na vikundi vya sanaa kila kona ya nchi, vingine vikipata umaarufu wa kitaifa na hata kimataifa.

Kulikuwa na vikundi vikubwa vya kitaifa, mfano, Kikundi cha Sanaa cha Taifa, kulikuwa na vikundi vya idara mbalimbali za serikali, vikundi vya sanaa vya mashirika ya umma, mashule, na vikundi vingi vya wasanii binafsi. 

Katika miji mingi, siku za Jumamosi ulikuwa huwezi kukosa kikundi cha sanaa za asili kikifanya maonyesho sehemu.  Vyuo  vya taaluma mbalimbali na hata vyuo vikuu vilikuwa na vikundi vya sanaa za asili. Vyuo vya ualimu vilikuwa na somo kwa ajili ya kufundisha sanaa kwa watoto, na kulikuwa na vyuo maalumu kwa ajili ya kutayarisha waalimu wa sanaa. 

Sikukuu hasa za serikali zilikuwa na vikundi vya ngoma kutoka makabila mbalimbali, ambayo mengi yalikuwa na tartaibu za kukutana mwisho wa wiki na kufurahia ngoma za kwao na watu waliweza kuhudhuria bure bila malipo. 

Mwalimu Nyerere hakuwa akizunguka na wasanii walio maarufu kibiashara, alijua kuwa kila anapo kwenda kuna wasanii kama alivyoeleza kwenye hotuba yake ya kuanzisha wizara ya sanaa. 

Kwa kuzunguka bila wasanii aliweza kuwaona wasanii wa kila aina ambao walikuwa chini ya uongozi wake, hilo pia lilikuwa ni jambo la kutia  hamasa kwa wasanii kuwa nao wanathaminiki kwa Rais wao. Je, ndoto ya Mwalimu ikoje katika zama hizi? Au tunaelekea kuwa wazungu weusi tena?