Siha. Viongozi wa vyama vya siasa na Serikali wametumia msiba wa aliyekuwa mgombea ubunge wa Chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Siha, Daudi Ntuyehabi (34), kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani, upendo na umoja, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Ntuyehabi alifariki dunia Oktoba 7, 2025, baada ya kushambuliwa na wananchi waliomtuhumu kuhusika katika tukio la kumjeruhi kijana mmoja wakati alipokwenda kuamua ugomvi wa mgombea huyo na mtu mwingine ambaye walikuwa wakidaiana fedha kwenye ‘grocery’ ya vinjwaji baridi.
Mwili wa mgombea huyo umeagwa leo Oktoba 11, 2025 nyumbani kwake, Kijiji cha Kilingi, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwao Kumlungwe, Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, kwa mazishi yatakayofanyika kesho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kmanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa watu wanane wanashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kujichukulia sheria mkononi na kumsababishia kifo mgombea huyo wa ubunge.
Akizungumza wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa marehemu, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dk Christopher Timbuka, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kujifunza kupendana, kusaidiana na kusameheana ili kuepusha matukio ya vurugu na mauaji.
“Katika msiba huu tujifunze kupendana, kusaidiana na kusameheana, tukiyafanya hayo, tutapunguza madhara makubwa yanayoigharimu jamii,” amesema Dk Timbuka.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Dk Christopher Timbuka akizungumza wakati wa mazishi ya aliyekuwa mgombea ubunge wa chama cha Wananchi (CUF) Jimbo la Siha, Daudi Ntuyehabi.
Aidha, ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na chama cha CUF kwa kumpoteza kiongozi wao katika kipindi hiki muhimu cha uchaguzi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza la Wazee Taifa (CUF), Arafa Mohamed, amewataka wananchi kuendeleza amani na upendo, akisisitiza kuwa misiba ni sehemu ya maisha na lazima jamii iendelee kushikamana.
“Amani ni kitu cha thamani sana katika maisha ya mwanadamu, tusiruhusu taharuki au maneno yanayoweza kuleta mtafaruku, kila kifo kina sababu, hivyo tuendelee kuwa na amani,” amesema.
Naye, Katibu wa CUF Jimbo la Siha, Adam Ramadhan, ametoa shukrani kwa vyama vingine vya siasa na viongozi wa serikali kwa kuungana nao katika shughuli za msiba huo.
“Tunashukuru CCM, ACT-Wazalendo na Chadema kwa kutoa rambirambi na ushirikiano, hii imeonyesha kuwa msiba si jambo la chama kimoja, bali la jamii nzima,” amesema Ramadhan.
Aliongeza kuwa chama hicho kimefarijika kuona viongozi wa vyama vingine, akiwemo mbunge wa jimbo hilo kutoka chama kingine, wakitoa msaada wa gari la kusafirisha mwili wa marehemu hadi Kigoma.
Kwa upande wake, Katibu wa ACT-Wazalendo Wilaya ya Siha, Giliard Mmari, amewataka wananchi kudumisha amani na mshikamano hasa katika kipindi hiki cha kampeni na uchaguzi mkuu.
“Tunaomba wananchi waendelee kudumisha amani, hasa wakati huu wa uchaguzi, ili kila mmoja apate fursa ya kumchagua kiongozi anayemtaka kwa utulivu,” amesema Mmari.
Aidha, ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, viongozi wa CUF na uongozi wa Wilaya ya Siha kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi chote cha maandalizi ya mazishi.