Msikie mkali wa kudanki Ligi ya Kikapu Dar

ILE Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ilimalizika wiki iliyopita ikishuhudia Dar City ikiondoka na ubingwa upande wa wanaume ilhali ule wa wanawake ambako DB Lioness ilitetea ubingwa ilioutwaa pia msimu uliopita.

Lakini, katikati ya bato la kuwania kubeba ubingwa kulikuwa na rekodi nyingi kali ambazo ziliwekwa na mastaa mbalimbali kuanzia wakali wa kuzuia, kushambulia na hata kutupia nyavuni.

Mbali na hao kulikuwa na wakali wa kudanki, yaani kufunga kiaina wakati mwingine wakimbembea katika mlingoti wa nyavu za goli na hii iliwaangukia kina Victor Michael na Clinton Best ndiyo wachezaji pekee walioweza kufanya hivyo mbele ya wachezaji wenzao kwa lugha ya mchezo huu wakiita ‘on your face’.

Michael anayeichezea Pazi alifanya yake katika mchezo wa robo fainali ya BDL dhidi ya Savio huku Best anayekipiga katika timu hiyo akifanya hivyo dhidi ya JKT kwenye mchezo wa fainali na wote wakidanki mara mbilimbili.

Katika Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), staa wa kudanki aliyeacha rekodi kali ni Shaquille O’neal aliyewahi kuichezea Los Angeles Lakers.

Kwa NBA imezoweleka kuwaona wachezaji wakidanki kwa mtindo wa kuruka juu haraka wanapokuwa katika eneo la kufunga na kutupia mpira nyavuni, huku wakiwa wamezongwa na wale wa timu pinzani, lakini kwa Tanzania mara nyingi hufanya hivyo wakiwa peke yao.

Kwa mujibu wa Michael kitendo cha kudanki mbele ya mastaa wengi wa timu pinzani, kinahitaji ujasiri na matumizi ya nguvu na kwamba bila kuwa na sifa hizo mtu hawezi kufanya lolote kwani ataishia kupoteza mpira.

Michael alilimbia Mwanasposti kwamba ufungaji mazoezi pekee kwa ajili ya tukio hilo ni suala muhimu, yakishirikisha wachezaji wengine eneo la mwisho kabla ya kufunga.

Nguvu anazozitaja Michael zinapaswa kujielekeza katika kuhakikisha kwamba hapigwi ‘push’ na kuondolewa kirahisi katika njia ya kuelekea mlingoti wa nyavu kwani wachezaji wa timu pinzani hujipanga vilivyo kuhakikisha kwamba hawafungwi pointi kwa njia ya kudanki inayotajwa kuwa kama dharau kwa wanaofungwa.

Akizungumzia ufungaji wa kudanki enzi zake, Shaquille aliyewahi pia kucheza Boston Celtics, Cleveland Cavaliers, Phoenix Suns, Miami Heat na Orlando Magic alisema uwezo wa kutupia mpira kwa kudanki ulitokana na mazoezi aliyokuwa akiyafanya nyumbani kwake na wachezaji chipukizi wa vyuo mbalimbali waliokuwa wakijifunza kikapu.

“Haikuwa rahisi, lakini mara zote dhamira ilikuwa ni kudanki, kudanki, kudanki ili kuwapa mashabiki kile kilichowafanya waingie uwanjani kututazama tukicheza. Huo ndiyo ukweli, vinginevyo ulimwengu wa kikapu ulifikia hatua ya kunitungia misamiati mingi ya namna nilivyokuwa nacheza,” alisema wakati fulani nyota huyo katika mahojiano na kituo kimoja cha redio huko Marekani.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipoanza kuvuma, makocha wa timu nyingi walitumia muda mwingi kumfanyia mazoezi na vikosi vyao ya namna ya kumdhibiti hususan kumdhibiti asiwafunge kirahisi na hapo ndipo walipoibuka na kile kilichoitwa “Hack-a-Shaq”, ikiwa ni mbinu ya kimchezo ya kufanya makosa dhidi ya mpinzani ili asiwafunge kirahisi.