Dar/mikoani. Mjadala kuhusu utulivu wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 umeendelea kupewa uzito na viongozi kutoka nyanja mbalimbali nchini.
Mada ya amani haijabaki kwenye mikutano ya kisiasa tu, imeingia ndani ya taasisi za kitaifa, vyombo vya dini, na hata kwenye maadhimisho ya kumbukumbu za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Taasisi kadhaa ikiwamo iliyoanzishwa na waliowahi kufanya kazi na Mwalimu Nyerere, wanazuoni na viongozi mbalimbali wakiwamo wa dini nao wamejiunga na wanaotoa wito huo.
Baadhi ya viongozi hao wamesisitiza kuwa uchaguzi usiwe chanzo cha mgawanyiko wa kijamii huku wengine wakihimiza kuhusu uwajibikaji wa vyombo vya usalama na kuheshimu Katiba, sheria na kanuni kwa kudumisha utulivu katika kipindi cha kampeni hadi muda wa uchaguzi.
Kongamano la kumbukizi ya Mwalimu Nyerere, lililofanyika leo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, limegeuka jukwaa muhimu la kutafakari si tu urithi wa Baba wa Taifa katika elimu na maendeleo, bali pia katika kulinda amani na umoja wa Watanzania kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa amani ni sharti kuu katika kufanikisha dira ya maendeleo ya Taifa hadi mwaka 2050.
“Rais Samia ameendelea kusisitiza kuwa hakuna maendeleo yatakayopatikana bila amani, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha tunadumisha misingi ya amani, umoja na mshikamano, kama alivyofundisha Baba wa Taifa.
“Na mimi niwahakikishie kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu, jitokezeni kusikiliza sera za wagombea ili ifikapo siku ya uchaguzi mkachague viongozi bora,” amesema Majaliwa.
Ameongeza kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni fursa muhimu kwa Watanzania kuonyesha ukomavu wa kisiasa kwa kushiriki kwa amani, bila mivutano wala vurugu.
“Nawasihi Watanzania washiriki katika kampeni na mikutano ya kisiasa kwa utulivu, wakisikiliza sera za wagombea na kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Wakili Albert Msando, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Serikali ya mkoa imejipanga kuhakikisha uchaguzi utafanyika kwa amani na usalama.
“Tutaendelea kulinda amani na utulivu kama sehemu ya kuenzi urithi wa Baba wa Taifa. Amani ni urithi wa thamani kuliko chochote, na ni jukumu letu sote kuilinda,” amesema Msando.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amegusi hoja hiyo, akisema hakuna maendeleo yatakayowezekana bila akisisitiza ushiriki wa amani katika uchaguzi mkuu ujao.
Kauli hizo zimeungwa mkono na viongozi wa vyuo vikuu na taasisi mbalimbali waliohudhuria kongamano hilo, akiwemo Profesa William Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyesisitiza kuwa fikra za Mwalimu Nyerere kuhusu umoja na amani ndizo msingi wa utambulisho wa Taifa.
Nje ya kongamano hilo, Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza limewaelekeza waumini wake kufunga kuanzia Oktoba 23 hadi 30, 2025, kuombea amani kuelekea uchaguzi mkuu.

Shekh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke akizungumza kwenye baraza la kiislamu lililofanyika mkoani humo. Picha na Saada Amir
Akizungumza wakati wa kikao cha baraza hilo, Shekh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amesema hatua hiyo inalenga kuiombea nchi amani na mshikamano wakati huu wa uchaguzi na baada ya matokeo.
“Tarehe 23 vituo vyetu watafunga hadi tarehe 30, siku ya matokeo ya uchaguzi. Ni maelekezo… watu watafunga. Hakuna kitu kigumu kama kukubali njaa, lakini watafunga kwa ajili ya nchi,” amesema Shekh Kabeke.
Ameongeza,”Hatuwezi kuridhia nchi hii ivunjike amani yake. Hii ni rasilimali waliyoitafuta wazee wetu kwa jasho na damu.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewataka wananchi na viongozi wa dini kuepuka lugha za uchochezi katika kipindi hiki cha uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja wa kitaifa.
Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (Juwakita), Zainabu Haruna amewahimiza wanawake Waislamu kushikamana katika azma ya kushiriki uchaguzi kwa amani na utulivu.
Naye Shekh Hassan Mchondo amesema tayari ameanza kuhamasisha Waislamu kwenye sala ya Ijumaa, waende wakapige kura na akalitaka Jeshi la Polisi siku hiyo lisitumie vifaru kulinda amani kwa kuwa Watanzania hawajazoea kuona vitu hivyo.
“Kwahiyo Watanzania wakiviona maana yake hawatoenda kupiga kura… Watanzania hawajazoea kuona vifaru. Jeshi la Polisi litumie mbinu bora za kulinda amani bila kuwafanya wananchi waogope kwenda kupiga kura,” amesema.
Kwa upande wake, Shekh wa Wilaya ya Ilemela, Abdulwarithi Bin Juma amesisitiza umuhimu wa kuzingatia utulivu baada ya kupiga kura akiwataka kufuata maelekezo ya kurudi majumbani mwao kusubiri matokeo baada ya kuchagua viongozi.
“Tunawatahadharisha waumini wetu wasijihusishe na maandamano. Baada ya kupiga kura, rudi nyumbani, tulinde amani yetu,” amesema.
Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, Paul Kimiti ametoa wito kuheshimiwa kwa mwezi huu wa Oktoba 2025 kwa kuwa mbali ya kuwa ni wa uchaguzi, pia ndio mwezi aliozaliwa Mwalimu Nyerere ambaye amekuwa kinara wa kudumisha amani na utulivu nchini.
Kimiti amesema hayo leo Jumamosi Oktoba 11, 2025 alipokuwa akitoa tamko lake rasmi kuhusu umuhimu wa kulinda amani nchini, wiki ya vijana na siku ya kilele cha kumbukumbu ya Nyerere.

Aliyekuwa Waziri wa zamani nchini, Lazaro Nyalandu akizungumza na viongozi wa dini mkoani Mwanza wakati wa baraza la kiislamu mkoani humo. Picha na Saada Amir
Amesema amani ndio msingi wa maisha, maendeleo na utu wa Watanzania na heshima hiyo ni kutoka kwa waasisi wa Taifa hili wakiongozwa na Baba wa Taifa, hivyo ni wajibu wananchi kuilida na kuienzi.
“Amani sio maneno, ni matendo, ni jinsi tunavyoheshimiana na jinsi tunavyoweka mbele maslahi ya Taifa kuliko masilahi binafsi.
“Pia tunavyoepuka kujihusisha na vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani kwani huu ndio utamaduni wa mtanzania,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Amani na Maridhiano Tanzania, Sheikh Alhad Mussa Salum amesema vijana wanapaswa kusikilizwa na kuelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya mitandao.
“Tunashuhudia kweli yanayoendelea mitandaoni, vijana wanazungumza, wengine ni matusi kabisa. Wakati huu sio wa kuzozana bali ni kuangalia kile vijana wanasema.
“Wasipuuzwe, maana si yote ni ya kipuuzi mengine wanasema ya msingi. Sote tupo jahazi moja, mmoja akitoboa mtumbwi, wote hatupo salama,” amesema Alhad alipozungumza na mwananchi.
Sheikh huyo amesema vijana nao wanapaswa kutumia hekima na busara mitandaoni, kwa kuwa taifa linahitaji maridhiano kwenye maeneo yenye tofauti badala ya matusi na marumbano.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya maaskofu na mashekhe ya haki, amani na maadili kwa jamii, Askofu William Mwamalanga amesema mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu ya kufikisha habari kwa haraka, lakini si wote wanaojua matumizi sahihi.
Lakini, amesema kumekuwa na ombwe la uelewa wa matumizi sahihi na yenye tija ya mitandao ya kijamii, ndio maana yanashuhudiwa matusi, mambo yanayopaswa kukemewa.