Othman: Viongozi wapimwe kwa wanavyojali wananchi

Unguja. Mgombea wa urais wa Zanzibar, kwa tiketi ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amewataka Wazanzibari kuwapima viongozi kwa vigezo mbalimbali ikiwemo kujali maslahi ya wananchi anaowaongoza.

“Mkitaka kupima kiongozi, mpime kwa kiasi hicho au kwa vigezo hivyo, maslahi makubwa ya wananchi ni haki katika nchi yao, ikifika mahali ukachukua haki ya mwananchi na kumpa mgeni unakiuka kiapo chako,” amesema Othman.

Othman amesema viongozi wakiingia katika ofisi za umma, wanakula kiapo kwa Mungu kwamba wanakwenda kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, bila uoga na kuweka mbele ya maslahi ya watu wanaokwenda kuwatumikia.

Othman maarufu ‘OMO’ ametoa ahadi hiyo leo Jumamosi Oktoba 11,2025 katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyikwa uwanja wa Kivumbi Jimbo la Amani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Ukiwa kiongozi wa nchi, uwe Rais, mwakilishi au mbunge, kazi yako kubwa ni kulinda maslahi ya nchi na maslahi ya wananchi, sio maslahi yako binafsi au familia yako,” ameeleza mgombea huyo.

Amesisitiza kuwa wajibu wa kwanza wa kiongozi ni kutunza haki za mwananchi, lakini hali tofauti ilivyo Zanzibar ndio maana kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wakidai kudhulumiwa haki zao ikiwemo ardhi.

Othman amewatoa hofu Wazanzibari, akiwataka kuwa amani kuelekea Oktoba 29, akidai ACT-Wazalendo kinaingia katika uchaguzi kikiwa na matumaini makubwa ya ushindi, kwa sababu waliomsimamisha ana sifa zote za kuongoza.

“Kila mahali tunasema tutairudisha Zanzibar kwenu(wananchi) ili kukomesha jeuri na ufisadi ili muwe na uwezo wa kuamua mambo yenu. Tutalinda haki zenu ambazo ndio wajibu mkubwa wa kiongozi,” ameeleza Othman.

Othman amesema kazi ya pili ya kiongozi ni kulinda mamlaka na rasilimali za nchi, akisema Zanzibar si masikini na Serikali atakayoiunda atahakikisha haki zote za kisiwa hicho zitarudi.

“Aliyezila atazitapika, lazima haki zirejeshwe ili Zanzibar irejeshe heshima yake,” amesisitiza Othman.

Katika mkutano huo, Othman amesema sera ya michezo imelenga kufufua sekta hizo ili kurejesha heshima ya Zanzibar iliyojengeka kwa miaka mingi iliyopita.

“Tutarudisha katika mpira wa miguu, kuogelea, tutarudisha heshima ya Zanzibar katika baadhi ya michezo ya asili kwa kuwawezesha. Tutarudisha heshima yetu kimataifa, kwa hiyo tutakuwa na Zanzibar ambayo vijana watatumia vipaji vyetu kwa ajili ya maendeleo,” amesema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Mansour Yusuph Himid amesema msingi wa Mapinduzi ni watu na ardhi, akisema hatua za mwanzo za mwasisi wa Taifa, Abeid Aman Karume(marehemu) zililenga watu.

“Mzee Karume alijenga maghorofa ya Michenzani na maeneo mengine ya Unguja na Pemba, akilenga kuwajenga kisaikolojia waliokuwa wengi kwamba na wao wanaweza kuishi kwenye nyumba za aina hiyo. Karume aliwajenga watu ili kujiamini, elimu bure, maji safi na salama bure.

“Leo hii hapa tulipo hiyo ardhi ipo? Leo Mzanzibari anakodishwa ardhi, Mapinduzi yamempa ardhi, heshima ya utu wake, Mapinduzi yamempa utajiri wa kumiliki ardhi.Tulipofika hapa hata mwananchi aliyekuwa na ardhi anaambiwa akodi, ndipo tulipofika,” amesema Mansour.

Mansour amedai kuwa Othman ndiye mgombea anayekubalika kwa sababu amewagusa Wazanzibari kwenye mioyo yao, ni mgombea anayejiuza si kujitembeza, pia maneno yake yanawagusa wananchi wakiamini atawalinda na kuwathamini.

“Niwaombe ndugu zangu tukaze buti, mtu kwa mtu, nyumba kwa nyumba. Niwaombe wagombea udiwani, ubunge na uwakilishi, kuacha mzaha waingie mitaani kufanya kazi, tutakuja kushangaa hata majimbo ya CCM yatakuja upinzani, hii ndio hali iliyokuwapo.

“Ndugu zangu wakati ni sasa, Othman ameturahisishia kazi, twendeni tukambebe mitaani hakuna kurudi nyumba. Wanaogombea jimbo la Kiembesamaki mshikamane, jimbo lipo wazi fanyeni kazi, ngoma imeshalala,” ameeleza Mansour.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Zanzibar Ismail Jussa amesema kwa namna kisiwa hicho kinastahili kuwa Singapore ya Afrika, kama ambavyo mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu).

“Niwaambie ndoto ya Maalim Seif kuigeuza Zanzibar kuwa Singapore ya Afrika, inakwenda kutimizwa na Othman Masoud Othman.Tutafanya hivyo kwa kuleta ubunifu Serikalini na kukomesha vitendo vya ufisadi,” ameeleza Jussa.