Ivory Coast imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya leo Ijumaa, Oktoba 10, 2025 kuibuka na ushindi mnono ugenini wa mabao 7-0 dhidi ya Shelisheli.
Katika mchezo huo ambao kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua alicheza kwa dakika zote 90, mabao ya Ivory Coast yamefungwa na Ibrahim Sangare, Emmanuel Agbadou, Oumar Diakite, Evanne Guessand, Yan Diomande, Simon Adingra na Franck Kessie.
Ivory Coast kwa ushindi huo imezidi kujikita kileleni mwa msimamo wa kundi F ikifikisha pointi 23 na inahitaji ushindi katika mechi yaje ya mwisho nyumbani dhidi ya Kenya, Jumanne, Oktoba 14, 2025 ili ifuzu Kombe la Dunia.
Katika Mchezo mwingine wa kundi hilo, Gambia ilipoteza nyumbani kwa mabao 3-4 mbele ya Gabon.
Nyuso za majonzi zimetawala nchini Afrika Kusini baada ya timu ya taifa ya nchi hiyo ‘Bafana Bafana’ kulazimishwa sare tasa nyumbani na Zimbabwe.
Sare hiyo imeiweka Bafana Bafana katika nafasi ngumu ya kufuzu Kombe la Dunia kwani imejikuta ikibaki katika nafasi ya pili kwenye kundi C ikiwa na pointi 15.
Na Benin imetumia vyema matokeo hayo ya sare ya Afrika Kusini kujiweka kileleni mwa msimamo wa kundi hilo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Rwanda.
Benin yenye pointi 17, sasa inahitajika kupata ushindi katika mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Nigeria ili ifuzu Kombe la Dunia.
Nigeria imepata ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Lesotho, matokeo ambayo yameifanya ifikishe pointi 14 na kushika nafasi ya tatu kwenye kundi C.