Sababu wanaokwenda kusoma Marekani kupungua

Dar es Salaam. Idadi ya wanafunzi wanaokwenda kusoma vyuo vikuu nchini Marekani imeshuka kwa asilimia tano, kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Usafiri na Utalii nchini humo.

Kushuka kwa idadi hiyo kunahusishwa na hatua za hivi karibuni za Rais wa Marekani, Donald Trump, kuongeza ukali wa ukaguzi kwa wanafunzi wanaoingia nchini humo kwa ajili ya masomo.

Takwimu za idara hiyo zinaonyesha kuwa idadi ya wageni wanaofika Marekani wakiwa na viza za wanafunzi imepungua kwa asilimia 19 kufikia Agosti mwaka huu, ikilinganishwa na mwezi kama huo mwaka 2024.

Hata hivyo, mawakala wanaosafirisha wanafunzi kutoka Tanzania kwenda nje ya nchi kwa ajili ya masomo wamesema ni vigumu kwa haraka kuona athari za mabadiliko hayo kwa wanafunzi wa Tanzania.

Mwakilishi wa taasisi inayohusika na kuwaandaa wanafunzi kusoma nje ya nchi, Darwin Educational Agency, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, amesema kuwa utaratibu wa udahili wa wanafunzi una mlolongo mrefu hadi kufanikiwa kusafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya masomo, jambo linalofanya athari za mabadiliko hayo kutoonekana mara moja.

“Utaratibu wa kudahili wanafunzi ni mrefu na una mambo mengi, zitakuwepo hizo athari lakini siyo kwa haraka,” amesema.

Kwa upande wake, Sylvester Mwashiuya, mwakilishi wa taasisi nyingine inayosafirisha wanafunzi kusoma nje ya nchi, Sangeni Abroad Education, amesema athari kubwa itakayoonekana ni wanafunzi kukosa fursa za masomo nchini Marekani.

“Kwa masharti au katazo kwa wanafunzi kuingia nchini humo, maana yake hatutakuwa na wanafunzi wengi wanaokwenda kusoma huko kwa ufadhili au kwa fedha zao wenyewe. Unapokosa fursa hiyo, maana yake wanafunzi wanashindwa kuchangamana na wenzao na kupata mtandao wa mawasiliano wa kupata fursa zaidi,” amesema.

Mbali na hayo, Mwashiuya amesema changamoto za upatikanaji wa viza kwa wanafunzi zinaweza pia kuleta athari za kidiplomasia, kwa kuwa hali hiyo inachukuliwa kama Marekani kuweka ukuta kwa watu wanaoingia nchini humo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Kitaifa ya Usafiri na Utalii, idadi ya wanafunzi imeendelea kupungua pia katika miezi ya Juni, Julai na Agosti 2025, kwa wastani wa asilimia 22 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.

Kutokana na hali hiyo, wadau wa sekta ya elimu wameonya kuhusu kupungua kwa udahili wa wanafunzi wa kimataifa, jambo linalotishia bajeti za taasisi za elimu pamoja na nafasi ya vyuo vya Marekani katika viwango vya kimataifa.

Ingawa bado haijafahamika ukubwa wa mabadiliko haya, takwimu mpya zinaashiria mwelekeo wa kupungua tena kwa udahili wa wanafunzi wa kimataifa nchini humo, baada ya kuanza kuimarika katika kipindi cha hivi karibuni kufuatia kushuka kwa kasi baada ya janga la Uviko-19.

Kulingana na taarifa kuhusu chanzo cha mapato ya vyuo vinavyotegemea ada za wanafunzi wa kimataifa, zaidi ya wanafunzi milioni 1.1 walikuwepo Marekani mwaka jana.

Hata hivyo, wanafunzi wengi waliokuwa na mipango ya kusoma Marekani hawakuweza kuingia nchini humo kutokana na ugumu wa kupata viza.

Mwishoni mwa Mei, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisitisha kwa muda ratiba za usaili wa visa kwa wanafunzi wa kigeni, hali iliyodumu kwa wiki tatu kabla ya kurejeshwa tena, safari hii ikiwa na masharti mapya ya kukagua akaunti za mitandao ya kijamii za waombaji wa visa husika.

Muda wa kusitisha huduma hiyo ulileta athari kwa utoaji wa visa kwa muhula wa masomo wa vuli, amesema Clay Harmon, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Usimamizi wa Usajili wa Wanafunzi wa Kimataifa.

Marufuku ya kusafiri na vizuizi vingine kwa nchi 19 vilivyotangazwa na utawala wa Trump mwezi Juni mwaka huu, viliongeza hali ya sintofahamu kwa baadhi ya wanafunzi wa kimataifa. Nchi nyingi zilizoathirika na marufuku hiyo zipo barani Afrika, Asia na Mashariki ya Kati.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa maeneo hayo yalishuhudia upungufu mkubwa wa wanafunzi wa kimataifa waliowasili Marekani kufikia Agosti mwaka huu.

Mchanganuo wa takwimu hizo unaonyesha Afrika wamepungua kwa asilimia 33, Asia kwa asilimia 24,huku India, ambayo ndiyo inayoongoza kwa kupeleka wanafunzi wengi Marekani, wakipungua kwa asilimia 45.

Takwimu hizo zinajumuisha wanafunzi wapya na wale waliokuwa wakirejea kwa masomo. Hata hivyo, baadhi ya wanafunzi waliokuwa tayari nchini Marekani waliepuka kusafiri nje wakati wa likizo ya kiangazi kwa hofu ya kukumbana na vikwazo vya kurejea nchini humo.

Mhitimu wa chuo mwaka 2022 nchini Iran, aliyetambulika kwa jina la Sara, amesema alikuwa na nafasi ya kujiunga na programu ya shahada ya uzamivu wa sayansi ya urejeshaji viungo (Physical Rehabilitation Science) katika Chuo Kikuu cha Iowa, akiwa amepata ufadhili kamili, lakini alilazimika kuahirisha safari.

Baada ya kukubaliwa katika programu hiyo kipindi cha masika, mahojiano yake ya visa yalisitishwa, na muda mfupi baadaye marufuku ya kusafiri iliyoihusisha Iran ilitangazwa.

Ingawa nafasi yake ya masomo imeahirishwa hadi mwaka ujao, Sara amesema ameanza kutuma maombi kwa vyuo vya Ujerumani.

Baadhi ya wanafunzi wa kimataifa na familia zao wamekuwa na wasiwasi kuhusu hali ya kisiasa nchini Marekani, hasa kutokana na msimamo mkali wa utawala wa Trump dhidi ya uhamiaji. Katika kipindi cha masika, serikali ya nchi hiyo iliwapokonya maelfu ya wanafunzi wa kimataifa hadhi yao ya kisheria ya ukaaji, jambo lililosababisha hofu kubwa kabla ya utawala wa Trump kubadili msimamo wake.

Aidha, Trump amewahi kutamka kuwa vyuo vikuu vinapaswa kupunguza utegemezi wao kwa wanafunzi wa kigeni na kuweka kikomo cha usajili wa kimataifa.

Zeynep Bowlus, mshauri wa elimu ya juu mjini Istanbul, Uturuki, amesema nia ya kusoma katika vyuo vya Marekani imekuwa ikipungua miongoni mwa familia anazofanya kazi nazo katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na gharama kubwa za masomo na mashaka juu ya thamani ya shahada kutoka Marekani.

Amefafanua kuwa mabadiliko ya sera nchini humo yanachochea zaidi wasiwasi huo.

“Najaribu kutoifanya ionekane ya kutisha sana, lakini wakati huohuo nawaambia ukweli wa hali halisi na vikwazo watakavyokutana navyo,” amesema Zeynep.

Wakati huohuo, taasisi za elimu katika nchi nyingine zimechukua fursa ya kuvutia wanafunzi wanaoweza kupunguza nia ya kusoma Marekani.

Idadi inayoongezeka ya wanafunzi kutoka China wameamua kubaki Asia, huku maombi ya kimataifa kwa vyuo vya Uingereza yakiongezeka kwa kasi.

Elisabeth Marksteiner, mshauri wa elimu ya juu mjini Cambridge, Uingereza, amesema anahamasisha familia zinazotazamia kujiunga vyuo vya Marekani kukabiliana na mchakato wa kuomba nafasi kwa tahadhari zaidi.

Ingawa visa ya mwanafunzi haijawahi kuwa uhakika, amesema ni muhimu zaidi kwa familia kuwa na mpango mbadala kwa wakati huu.

“Nadhani wengi wana dhana kwamba mambo yataendelea kama zamani,” amesema Marksteiner.