Dodoma. Serikali imetangaza nafasi 41,500 za ajira kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na kuwataka Watanzania wenye sifa kuchangamkia fursa hizo haraka.
Ajira hizo ni kwenye kada za elimu nafasi 12,176, sekta ya afya ngazi ya serikali za mitaa (10,280), kilimo (470), mifugo (312), uvuvi (47), ulinzi inayohusisha Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uhamiaji ni ajira 7000.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jumamosi Oktoba 11, 2025 kwenye Ofisi za Utumishi Mtumba Jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi amesema ajira hizo ni zilizotengwa kwa mwaka 2025/2026.
Mkomi ameiagiza Sekretarieti ya ajira kukamilisha mchakato huo kwenye nafasi ambazo hazijajazwa mwaka wa fedha 2024/25 ambapo ni ajira 45,000 na za mwaka 2025/26 ifikapo Novemba mwaka huu.
”Hadi kufikia Novemba mwaka huu tunataka vibali vyote vya ajira 86,500 vilivyotolewa kwa mwaka 2024/25 na mwaka 2025/26 ziwe zimejazwa na waliopata ajira hizo kuanza kazi mara moja ili kuziba upungufu wa watumishi uliopo nchini,” amesema Mkomi.
Katibu huyo ameagiza barua za wote watakaopata kazi kupitia kwenye akaunti zao za ajira portal badala ya kuzifuta Dodoma ili kupunguza usumbufu na gharama kwa watakaopata ajira mpya.
”Pia usaili wa wanaoomba ajira serikalini ufanyike kwenye mikoa husika na barua zao za ajira zipitie kwenye akaunti zao zilizopo kwenye ajira portal ili kuondoa usumbufu na gharama za kuja Dodoma na kurudi kwenye vituo vyao vya kazi walivyopangiwa,” amesema Mkomi.
Mbali na hilo amesema mpaka sasa Serikali ina upungufu wa watumishi wa umma takribani 280,000 na kwamba Serikali inajitahidi kupunguza ombwe hilo kwa kuendelea kutoa vibali vya ajira mahali penye upungufu.
Mkomi ametoa taarifa ya tathmini ya wiki ya huduma kwa wateja kwa watumishi wa umma ambapo jumla ya watumishi 312 walijitokeza kuhudumiwa na changamoto kubwa ilikuwa ni matumizi ya mfumo wa Pepmis na Pipmis, hata hivyo walihudumiwa.