Sowah, Pantev kuna kitu kipya kinasukwa Simba

KUNA kitu mshambuliaji wa Simba, Jonathan Sowah amemshtukia Kocha Dimitir Pantev tangu ametua katika kikosi hicho, kisha akawatuliza mashabiki wa klabu hiyo akiwaambia kuna hesabu kali zinatengenezwa ili kuwa na timu imara yenye ushindani mkubwa, huku mwenyewe akijipanga na suala zima la kufunga mabao.

Pantev ambaye ametua Oktoba 4, 2025 baada ya kutambulishwa Simba akitokea Gaborone United ya Botswana akiwa ndiye mrithi wa Fadlu Davids aliyeondoka baada ya mchezo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, tayari ameanza kazi ya kukinoa kikosi hicho.

Katika maandalizi ya kukiweka imara kikosi cha Simba, Pantev, Oktoba 9, 2025 alikiongoza kushinda mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan ikiwa ni mechi ya kirafiki, huku Sowah akitupia bao la ushindi. Jean Charles Ahoua akifunga la kwanza. La Al Hilal, mfungaji Adama Coulibaly.

Akizungumza na Mwanaspoti, Sowah amesema baada ya mechi hiyo ya kirafiki dhidi ya Al Hilal, anaona kikosi chao kinakwenda kuwa tishio kutokana na namna kocha huyo amaeanza hesabu zake.

Sowah raia wa Ghana, amesema Pantev ni kocha wa soka la ushindi na anataka kuona timu hiyo inamiliki mpira muda wote, pia inafunga mabao.

Mshambuliaji huyo ambaye alifunga bao moja kwenye ushindi dhidi ya Al Hilal ya Sudan, amesema Pantev anataka kuona anafunga mabao akiwa kama mshambuliaji.

Kwenye mechi hiyo Sowah alicheza kwa dakika 35 za kipindi cha pili kisha akafunga bao la ushindi, baada Ahoua kufunga la kwanza, huku Simba ikitoka nyuma na kutengeneza ushindi huo, mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Pantev tangu aanze kazi ndani ya klabu hiyo.

“Huyu ni kocha mzuri sana, Simba ni timu inayotaka ushindi wakati wote na yeye (Pantev) anataka wachezaji tucheze kwa kujiamini na tuwashambulie wapinzani,” amesema Sowah ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Singida Black Stars iliyomleta nchini kipindi cha dirisha dogo la usajili msimu wa 2024-2025.

“Mimi jana (Oktoba 9, 2025) wakati naingia uwanjani aliniita akaniambia, ‘Sowah nataka ufunge mabao, hiyo ndio kazi yako kama mshambuliaji’ na namshukuru Mungu nikafunga, mechi ilivyoisha akaniambia nilichofanya ndio anachotaka washambuliaji tufanye.

“Mashabiki wasubiri, wampe nafasi afanye kazi yake kwani namna ninavyomwona anachotaka kifanyike kitaipa nguvu kubwa timu yetu kwenye mechi zetu.”

Sowah aliongeza, anajipanga kuendelea kufunga zaidi ili kujitengenezea nafasi mbele ya kocha huyo raia wa Bulgaria.

“Mimi ni mchezaji na mshambuliaji, siwezi kumwambia kocha anipe muda gani uwanjani, unaona alinipa dakika 35 za mwisho na nikaenda kufunga bao, hili ndiyo nataka kulifanya, hata nikipata dakika tano basi nifanye kitu tofauti,” amesema Sowah.

Tangu atue Simba msimu huu, Sowah kwenye mechi za mashindano amefanikiwa kufunga bao moja kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate katika Ligi Kuu Bara, akiwa ameshacheza mechi tatu zikiwemo mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu uliopita, mshambuliaji huyo katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara alizocheza kuanzia alipotua Singida Black Stars Januari 2025, alifunga mabao 13, akimaliza kwenye nafasi ya tatu ya wachezaji wenye mabao mengi nyuma ya kinara Ahoua (16) na Clement Mzize (14), pia akiwa sawa na Steven Mukwala, Leonel Ateba na Prince Dube.