Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limezitaka serikali na washirika duniani kote kuongeza juhudi za kuwalinda na kuwawezesha wasichana balehe, hasa wanaoishi katika maeneo yenye migogoro, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Msichana.
Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Diene Keita amesema mamilioni ya wasichana bado wanakabiliwa na hali ngumu za vita, ukimbizi na misukosuko ya kiuchumi hali zinazowanyima haki ya kupata elimu, huduma za afya na haki za msingi za kibinadamu.
Amesema kila msichana ana haki ya kujikubali alivyo na kuchagua anachotaka kuwa.
“Kwenye safari yake kuelekea utu uzima, lazima alindwe, aheshimiwe na apewe nafasi ya kustawi. Matamanio yake kuhusu maisha yajayo yasikilizwe na yahimizwe, huku haki na chaguo lake zikilindwa,” amesema Diene.
Kwa mujibu wa UNFPA, karibu nusu ya vijana duniani wanaishi katika nchi zinazokumbwa na viwango vya juu au vya juu zaidi vya migogoro ya kivita.
Katika mazingira kama hayo, wasichana balehe mara nyingi ndio wa kwanza kupoteza fursa ya kwenda shule, kupata huduma za afya na huduma muhimu za afya ya uzazi na ujinsia.
Diene amebainisha kuwa hali ya kutokuwa na usalama na ugumu wa kiuchumi huongeza hatari kwa wasichana kukumbwa na unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za utotoni. Hata hivyo, licha ya changamoto hizo, wasichana wengi wanaonyesha ustahimilivu na uongozi wa kipekee.
“Wanataka usalama, heshima na haki za kibinadamu, wakitumia uzoefu wao wenyewe kudai kukomeshwa kwa vitendo hatarishi kama vile ukeketaji,” amesema. “Wanalia kwa ajili ya amani kwa familia zao, wenzao na jamii zao.”
UNFPA imebainisha kuwa inaendelea kusaidia wasichana kupitia vituo rafiki kwa vijana katika nchi 32 zilizoathiriwa na migogoro, ambavyo hutoa taarifa muhimu, ushauri wa kisaikolojia, mafunzo ya ufundi na nafasi za vijana kueleza maoni yao.
Mshiriki mmoja wa mpango huo alieleza nguvu ya mabadiliko inayotokana na programu hizo, akisema: “Marafiki zangu na mimi katika kituo cha vijana tumejifunza na kujibadilisha ili tuweze kusaidia kizazi kijacho. Hatutaki waone au wapitie yale tuliyopitia sisi.”
Diene amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika mashirika yanayoongozwa na wasichana balehe na wanawake vijana, akiongeza kuwa UNFPA inaendelea kushirikiana na harakati zinazoongozwa na vijana zinazotetea afya, haki, usawa wa kijinsia na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Wakati msichana anapochukua hatua kukabiliana na changamoto zinazomkabili, lazima awe na uhakika kuwa dunia inasimama pamoja naye,” amesema. “Tujitolee, katika Siku hii ya Kimataifa ya Msichana, kuendeleza afya ya uzazi na haki za wasichana balehe popote walipo.”
Wakilishi wa vijana kuhusu afya ya uzazi – EANNASO, Letisia Mswaki ametaja ukatili wa kijinsia hasa vipigo, ndoa za utotoni hasa mikoa ya Dodoma, Tabora, Mara na Manyara, ukosefu wa huduma rafiki za afya ya uzazi hasa kukosa pedi na kutembea umbali mrefu kufika wakati wa kwenda mashuleni ni miongoni mwa vikwazo kwa wasichana,
Akitoa mapendekezo yake, Letisia amesema ni muhimu kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii hasa wazazi ili kuhakikisha wasichana wanapata elimu ya afya ya uzazi kuanzia ngazi ya nyumbani (malezi), kijamii na hadi kitaifa.
“Tuepuke mila potofu ambazo ni chochezi katika kusababisha ukatili kijinsia na ndoa za utotoni. Kuipa jamii elimu juu ya umuhimu wa kumuelimisha msichana na kumpa nafasi katika ngazi ya maamuzi na kiuongozi.
“Kubadilishwa kwa sera mbalimbali katika nyanja za elimu, afya na uchumi ambazo zitajikita katika kumlinda msichana na kumpa haki zake za msingi, pia muhimu kupangwa kwa bajeti inayojikita katika mlengwa wa kijinsia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu, afya, maji na uchumi,” amependekeza Letisia.