::::::::::::::::
Utafiti unaofanyika katika mradi wa kimkakati wa Eyasi Wembere unaolenga kutafuta mafuta na gesi katika bonde la ufa la Afrika Mashariki umeonesha matumaini makubwa ya kupatikana kwa Mafuta na Gesi katika bonde hilo.
Hayo yamebainika wakati Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mkoani Arusha wilaya ya Karatu
“Kazi za utafiti wa mradi huu zimeanza mwaka 2015, tumekuwa tukikusanya data mbalimbali zinazohusiana na uwepo wa mafuta na gesi ambapo baada ya ukusanyaji, data hizo zilitumika kubainisha miamba tabaka ambayo ina mafuta na tukajiridhisha kwamba katika eneo hili la bonde ipo miamba ambayo inaweza ikahifadhi mafuta”.Amesema Dkt. Mataragio.
Dkt. Mataragio ameeleza kuwa, data za awali za utafiti zilizoanza 2015 kwa njia ya ndege na uchorongaji visima vifupi ambpo ziligharimu takribani shilingi bilioni nane.
Aliendelea kufafanua kuwa data za awamu ya kwanza kwa njia ya mitetemo zenye urefu wa kilometa 260 ziligharimu takribani shilingi bilioni 10.
Aidha, shughuli za utafiti katika awamu ya pili zitahusisha eneo la kilomita 914 zitagharimu shillingi bilioni 43 ambapo kilomita 430 ndio zimekamilika sawa na asilimia 47.
Akizungumzia faida zitakazopatikana nchi ikipata mafuta kutoka eneo hilo ni pamoja na uhakika wa uwepo wa mafuta na kupunguza gharama za ununuaji wa mafuta nje ya nchi.
“Tutaweza pia kutunza akiba ya fedha za kigeni ambazo zinatumika kwa ajili ya kuagiza mafuta nje ya Nchi”. Ameongeza Dkt. Mataragio
Katika hatua nyingine, Dkt. Mataragio amesema kuwa kutoka kuanza kwa mradi mwaka 2015 takribani asilimia 90 ya wanaotekeleza mradi ni watanzania.
Baada ya ukaguzi wa mradi huo, Dkt. Mataragio ameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Mkandarasi kampuni ya AGS kuhakikisha kuwa wanakamilisha mradi kabla ya mwezi Aprili na kazi ziendelee hata kipindi cha mvua.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utafutaji Uendelezaji na uzalishaji Mafuta na Gesi kutoka TPDC, Mjiolojia Paschal Njiko amesema TPDC inafanya utafiti katika bonde hilo kwa kushirikiana na Mkandarasi mzawa kampuni ya African Geographical Services (AGS).
Njiko amesema TPDC imepokea maagizo yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu na itahakikisha inamsimamia Mkandarasi ili kuhakikisha utafiti wa awamu ya pili unakamilika kwa wakati.
Naye, Mwenyekiti wa kampuni ya AGS ambayo ni Mkandarasi anayesimamia utafiti katika Bonde la Eyasi Wembere, Salum Haji amesema wanatambua unuhimu wa mradi huo kwa kwa taifa hivyo watahakikisha utafiti unakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa.
Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa mradi wa Bonde la Eyasi Wembere, Biru Benjamini amesema “kupitia mradi huu sisi vijana tuliokuwa mtaani tumenufaika na ajira na pia kupata ujuzi.”