Vigingi vitano vinavyomkabili mtoto wa kike

Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wamepaza sauti wakihitaji mabadiliko ya kisera, kikanuni na kisheria katika maeneo makuu matano, waliyoyataja kuwa vikwazo kwa mtoto wa kike kufikia malengo, ikiwemo uwekezaji hafifu wa elimu ya afya ya uzazi.

Oktoba 11 kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike, ambayo kaulimbiu ya mwaka huu inasema, ‘Mimi ni msichana, Kinara wa Mabadiliko kwa Tanzania tuitakayo 2050.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Oktoba 11, 2025 wameyataja maeneo hayo kuwa ni upungufu wa haki ya kupata huduma za afya ya uzazi, ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni na ulinzi hafifu wa mtoto wa kike kwa wazazi wote wawili.

Wakili na mtetezi wa haki za wanawake na watoto wa kike, Walta Carlos amesema licha ya kuwa kaulimbiu ya mwaka huu kuakisi msichana kinara, kuna mambo mengi yanapaswa kufanyiwa kazi ili kuleta wepesi kwa msichana kuzifikia ndoto zake.

Amesema mimba na ndoa za utotoni, sheria kandamizi, mila na desturi bado ni kikwazo kwa jamii nyingi nchini.

“Pamoja na kwamba tunamtaka msichana kinara 2050 kuna vikwazo ambavyo huyu binti tunayemtaka anaweza akakosa fursa,” amesema.

Walta ameitaja sheria ya ndoa za utotoni kuwa kikwazo kikubwa, na kwamba mawakili kwa muda mrefu wamekuwa wakipambana nalo.

Pamoja na hayo ameutaja mwongozo wa kuwarejesha shule wasichana waliojifungua ndani ya miaka miwili kuwa una changamoto katika utekelezaji.

“Kwenye utekelekezaji tukaanza kuziona changamoto, hauna nguvu hivyo tunahitaji kupata sheria. Itengenezwe sheria rasmi ambayo itaidhinisha binti arudi shule, sababu kuna Tangazo la Serikali ya mwaka 2002 GN625 yenyewe ilikuwa inaonyesha kwamba kupata ujauzito ni kosa na kinyume na maadili,” amesema.

Amesema mabinti wanaorejea shule wanakumbana na unyanyapaa kutoka kwa wanafunzi wenzao, jamii, walimu wao kwani wengine wanaona wataenda kuwaharibu wenzao.

“Sheria imeruhusu binti arudi shule lakini ana hatari kubwa ya kupata ujauzito wakati mwingine, bado miundombinu na mwingine hana wa kumwachia mtoto kuwepo miundombinu akaweza kutoka, akanyonyesha na kurudi kuendelea na masomo,” amesema na kuongeza huduma ya kisaikolojia kabla ya kurejea masononi ni muhimu.

Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA – HC), Dk Ntuli Kapologwe ametaja kikwazo kikubwa kuwa ni ulinzi hafifu wa mtoto wa kike kutoka kwa wazazi wote wawili, “Baba na mama. Pia bado uwekezaji ni hafifu wa elimu ya uzazi kwa mtoto wa kike.”

Wakilishi wa vijana kuhusu afya ya uzazi – EANNASO, Letisia Mswaki ametaja ukatili wa kijinsia hasa vipigo, ndoa za utotoni hasa mikoa ya Dodoma, Tabora, Mara na Manyara, ukosefu wa huduma rafiki za afya ya uzazi hasa kukosa pedi na kutembea umbali mrefu kufika wakati wa kwenda shuleni ni miongoni mwa vikwazo kwa wasichana,

Akitoa mapendekezo yake, Letisia amesema ni muhimu kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa jamii hasa wazazi ili kuhakikisha wasichana wanapata elimu ya afya ya uzazi kuanzia ngazi ya nyumbani (malezi), kijamii na hadi kitaifa.

“Tuepuke mila potofu ambazo ni chochezi katika kusababisha ukatili kijinsia na ndoa za utotoni. ⁠Kuipa jamii elimu juu ya umuhimu wa kumuelimisha msichana na kumpa nafasi katika ngazi ya maamuzi na kiuongozi.

“⁠Kubadilishwa kwa sera mbalimbali katika nyanja za elimu, afya na uchumi ambazo zitajikita katika kumlinda msichana na kumpa haki zake za msingi, pia muhimu kupangwa kwa bajeti inayojikita katika mlengwa wa kijinsia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu, afya, maji na uchumi,” amependekeza Letisia.

Wakati huohuo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) limezitaka Serikali na washirika duniani kote kuongeza juhudi za kuwalinda na kuwawezesha wasichana balehe, hasa wanaoishi katika maeneo yenye migogoro, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Msichana.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA, Diene Keita, alisema kila msichana ana haki ya kujikubali alivyo na kuchagua anachotaka kuwa, “Kwenye safari yake kuelekea utu uzima, lazima alindwe, aheshimiwe na apewe nafasi ya kustawi. Matamanio yake kuhusu masha yajayo yasikilizwe na yahimizwe, huku haki na chaguo lake zikilindwa.”