WASITHUBUTU KUFANYA FUJO,KIBATI KIKIPASUKA TU TUKO NAO- RAIS SAMIA

Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Bariadi

RAIS Dk.Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama amewatoa watanzania kutokana na uwepo watu wanaotisha kuwafanya watu wasitoke Oktoba 29 kwenda kupiga kura ambapo amesema watu hao wasithubutu kibati kikipasuka tu Serikali iko nao.

Dk.Samia ambaye kwa sasa ni mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameyasema hayo akiwa katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu ambako anaendelea na mikutano ya kampeni kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu.

“Na hapa niseme niwatoe hofu , kuna watu wanatishatisha kuwafanya watu wasitoke tarehe 29 kwenda kupiga kura.Nataka kuwaambia ninayezungumza hapa ni Amiri Jsshi wa nchi hii.

“Nataka kuwaambia wasithubutu kibati tu kikipasuka sisi tuko nao tumejipanga vizuri ,hivyo wananchi tokeni kapigeni kura rudini nyumbani kapumzike hakuna hofu wala hakuna kuogopa, tokeni mkapige kura tarehe 29.”

Awali akizungumza na maelfu ya wananchi wa Bariadi waliokuwa wakimsikiliza katika mkutano huo ,Mgombea Urais Dk.Samia amesema Serikali katika miaka mitano iliyopita imefanya mkazo kubwa ya kuleta maendeleo katika maeneo yote.

“Pia tumefanyakazi kubwa katika maeneo yote ikiwemo ya miundombinu ya barabara , anga,usafiri wa  maji kwa kujenga bandari na vyombo vya usafiri

“Lakin tumefanya kazi kwenye ujenzi wa reli kule Mwanza kuna reli ya SGR ambapo sehemu ya reli itapita hapa Simiyu eneo la Maswa wilayani Maswa .”

Pia alısema kuna reli ya SGR itatoka Tanga,Moshi ,Arusha  mpaka Musoma na kwa Mkoani Simiyu itapita Meatu,Itirima na Bariadi na huko kote ambako inapita  itakuwa na vituo vya kushusha na kupakia.

“Nimesema hivyo kwasababu hii ni fursa ya biashara lakini ni ajira kwa vijana wetu kwasababu katika vituo vile kutakuwa na maeneo ya biashara hoteli.

“Lakini Serikali itajenga maghala ya kuhifadhia biadhaa zitakazosafirishwa na reli ya hiyo. Kwahiyo hizo ni fursa za ajira ni kazi kwa vijana wetu hivyo mkae tayari kutumia fursa hizo

“Kwa ujumla Chama Cha Mapinduzi tumedhamiria kufanya kazi , tumefanya kazi mmeona na tunaamini tunaweza kufanya tena kazi kipindi  cha pili cha awamu ya sita kazi ya kuonekana.Kwahiyo niombe mtuchague.”