Aaron Kalambo aanika malengo mapya

KIPA wa Transit Camp, Aaron Kalambo amesema ni muda sahihi wa kurejesha kiwango chake na timu hiyo ya maafande, baada ya nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu, akitokea Coastal Union kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara.

Nyota huyo amejiunga na Transit Camp baada ya kuachana na Coastal Union, ambayo hata hivyo, hakupata muda zaidi na timu hiyo wa kucheza msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, kutokana na kusumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara ya goti lake.

“Malengo yetu ni kufanya vizuri na kurejesha heshima yangu iliyojengeka kwa mashabiki, sikuwa na muda mzuri na Coastal Union, ingawa kwa sasa naangalia yaliyo mbele kwetu kwa maana ya kukipambania kikosi chetu kijumla,” amesema Kalambo.

Akizungumzia ushindani wa Ligi ya Championship msimu huu, amesema timu zote 16, zimejipanga vizuri kwa sababu ya uwepo wa wachezaji bora na wazoefu wenye hadhi ya Ligi Kuu, hivyo, sio rahisi hata kidogo kama wengi wao wanavyofikiria.

Nyota huyo amejiunga na Transit Camp baada ya kuachana na Coastal Union aliyojiunga nayo kwa mkataba wa miezi sita tu, akitokea Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, huku akiwahi kucheza pia kikosi cha ‘Walima Zabibu’, Dodoma Jiji.