Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir, ameelezea namna atakavyopata fedha za kumlipa kila Mzanzibari Sh500,000 kila mwezi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti matumizi makubwa ya Serikali atakayoiunda, hususan misafara mikubwa ya Rais.
Amesema iwapo akipewa ridhaa na Wazanzibari ya kuingia Ikulu, magari ya Rais hayatazidi sita ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha za Serikali, na fedha hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya wananchi.
Pamoja na kudhibiti matumizi ya Serikali, chama hicho kimeainisha vipaumbele muhimu katika sekta tisa vitakavyowekewa mkazo na kuwezesha ukusanyaji wa mapato, lengo ni kuhakikisha makusanyo hayashuki chini ya Sh1.7 trilioni kwa mwezi.
Ameir ametoa kauli hiyo leo, Jumapili Oktoba 12, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya kampeni na kufafanua namna atakavyopata fedha hizo, akisema kumekuwa na maswali mengi ya namna atakavyopata fedha za kumlipa kila Mzanzibari kila mwezi.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama Cha Makini, Ameir Hassan Ameir akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya kampeni zake na kutoa ufafanuzi wa jinsi atakavyopata Sh500000 za kumlipa kila Mzanzibari kwa mwezi. Picha na Jesse Mikofu
“Kwa mwezi tutahakikisha tunakusanya Sh1.7 trilioni, na kwa makadirio ya wananchi wa Zanzibar ni milioni mbili, kwa hiyo ukigawa Sh500,000 kwa mwezi kwa kila Mzanzibari, tutatumia Sh1 trilioni na Sh700 bilioni zitawekwa kwenye mfuko wa Serikali kwa ajili ya maendeleo,” amesema Ameir.
Hata hivyo, kwa mujibu wa sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina jumla ya wananchi 1,889,773.
Amesema chama hicho kitatoa mgawo mkubwa wa makusanyo kwa wananchi kuliko matumizi ya Serikali kwa sababu wananchi ndio wamiliki wa nchi na rasilimali zilizomo.
Kwa mujibu wa Ameir, kuna sekta tisa ambazo wataziwekea mkazo na kukuza makusanyo, ikiwa ni pamoja na utalii, uvuvi, kilimo hai, elimu na ujuzi, miundombinu ya uchumi, na kujenga viwanda vidogo na vya kati.
Sekta nyingine ni kuvutia uwekezaji wa ndani na nje, kuboresha utawala bora na kupambana na rushwa, pamoja na kuweka mifumo ya kidijitali.
“Tutabadilisha mambo kwa vitendo, si maneno. Tutaweka sheria kali mpya, wizi wa fedha za umma utakuwa uhalifu wa uhaini, adhabu yake itakuwa kifungo kisichopungua miaka 15 na kufilisiwa mali zote. Viongozi watakaokutwa na hatia hawatashika madaraka milele,” amesema.
Akifafanua sekta moja moja namna watakavyofanya kazi, mgombea huyo amesema katika sekta ya utalii watakuza utalii wa kiutamaduni, kiikolojia na kihistoria, badala ya utalii wa fukwe pekee ambao ndio unapewa kipaumbele kwa sasa.
“Kuongeza ubora wa huduma za hoteli, usafiri na usalama kwa watalii na kuwekeza katika masoko mapya ya Asia, Mashariki ya Kati na ndani ya Afrika,” amesema.
Kwa upande wa sekta ya uvuvi, Ameir amesema watawekeza katika zana za kisasa na uvuvi wa bahari kuu, na kuongeza thamani kwa bidhaa za samaki kwa kusindika na kufungasha bidhaa.
Katika kuwekeza elimu na ujuzi, amesema watazalisha vijana kwenye fani zinazouzika sokoni kama teknolojia na biashara, na kukuza elimu ya ujasiriamali kwa kujenga vyuo vya amali.
“Kuboresha miundombinu ya uchumi, barabara, umeme, maji safi na salama, bandari na mitandao bora ya mawasiliano,” amesema Ameir.
Kingine, Ameir amesema wataboresha mazingira ya uwekezaji kwa kupunguza urasimu, kuweka uwazi na kutoa motisha kwa wawekezaji, huku wawekezaji wa ndani wakipatiwa mikopo yenye riba nafuu.

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama Cha Makini, Ameir Hassan Ameir akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tathmini ya kampeni zake na kutoa ufafanuzi wa jinsi atakavyopata Sh500000 za kumlipa kila Mzanzibari kwa mwezi. Picha na Jesse Mikofu
Katika eneo la utawala bora na kupambana na rushwa, Ameir amesema iwapo akipata ridhaa, atahakikisha matumizi sahihi ya rasilimali na uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali, sekta za umma na binafsi.
Amesema ataanzisha kadi za kidijitali kudhibiti mapato ya Serikali na kutoa huduma kwa wananchi kwa uwazi, pamoja na kuanzisha kadi za kidijitali kwa maeneo yote ya maegesho ya magari na vyoo vya umma.
Akizungumza kuhusu tathmini ya kampeni tangu zimeanza, Ameir amesema inaonesha Wazanzibari wamempokea vyema kutokana na sera zake, na mpaka sasa anaamini atashinda wagombea wengine wote 10 anaoshindana nao.
Kikubwa kinachompa jeuri, amesema, ni namna ambavyo ameendesha kampeni zao kwa kuwafuata wananchi katika maeneo yao, sio wananchi kuwafuata wagombea.
“Sisi tunakwenda kwenye maeneo yao na tunahakikisha walewale wa eneo husika ndio tunaongea nao, sio kuwasomba watu na magari kuwatoa maeneo mengine. Na sera zetu, hasa hii ya kumpa Mzanzibari Sh500,000, imependwa sana,” amesema.
Naye Katibu Mwenezi Taifa wa chama hicho, Fahmi Khalfan Abdalla, amesema kila chama kina vipaumbele vyake, lakini vipaumbele vya Makini vimewakosha watu wengi, hivyo wanaamini watachaguliwa na kuingia Ikulu.