“Sasa mama Faustin naona nikuwache, umeshapata mwenzako wa kuzungumza naye. Mimi naondoka. Tutakapokuhitaji tutakupigia simu.”
Nikarudi kwenye gari na kuondoka. Kwa tabia za wanawake nilijua watazungumza kila kitu lakini kitu muhimu niichokijali ni kuwa mwanamke huyo atakuwa pale kwa mwanawe ingawa sikuwa na uhakika kwamba angekaa kwa muda mrefu kabla ya kurudi alikotoka kwani shauri la mwanawe lingechukua muda mrefu.
Niliporudi ofisini nilimpigia simu afisa upelelezi nikamueleza kila kitu kilichotokea. Akanisisitizia kuwa niharakishe mashitaka ya Faustin ili yapelekwe kwa mkurugenzi wa mashitaka.
Baada ya wiki moja jalada ambalo lilipelekwa kwa mkurugenzi wa mashitaka lilikabidhiwa kwa mawakili wa serikali ili kumfikisha mahakamani Faustin.
Faustin akapelekwa mahakamani na kusomewa shitaka la mauaji ya watu wanne ambao aliwanyonga.
Kesi ilianza katika mahakama ya hakimu mkazi kabla ya kuhamishiwa mahakama kuu.
Faustin alipoulizwa kama anakiri kosa au anakana. Alisema.
“Unakiri kosa kwamba uliwanyonga watu wanne?” mheshimiwa jaji alimuuliza.
“Ndiyo ninakiri kosa kwamba niliwaua watu wanne kwa kuwanyonga.”
Jaji akaandika maelezo ya Faustin kwenye faili lake. Baada ya kuandika alimwambia wakili wa serikali.
“Japokuwa mshitakiwa amekiri kosa ni lazima upande wa mashitaka ulete mashahidi ili wathibitishe hapa mahakamani kuwa mshitakiwa ametenda kosa hilo na mahakama ijiridhishe kwamba kweli kosa hilo limetendeka.”
Jaji aliendelea kutaja kesi mbalimbali za nyuma ambapo washitakiwa walikiri makosa kwa kutojua sheria lakini baada ya ushahidi kutolewa ikaonekana kuwa hawakutenda kosa kisheria.
Wakili wa mshitakiwa ambaye aliwekewa na serikali alikubali kuwa ushaidi huo uletwe mahakamani ili pande zote ziusikie.
Upande wa mashitaka ukaahidi kupeleka mashahidi hao kesi itakapoitishwa tena.
Kesi ikaahirishwa kwa wiki nne na Faustin akarudishwa mahabusu.
Mimi nilikuwa shahidi muhimu katika kesi hiyo na niliamini kama mshitakiwa ameamua kukiri kosa mbele ya jaji hatutakuwa na kazi kubwa ya kuithibitishia mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa aliloshitakiwa nalo.
Kwa vile mshitakiwa aliamua mwenyewe kukiri kosa nilijua tusingekumbana na hoja za wakili wake kupingana na ushahidi wetu. Mara nyingi hoja za mawakili wa utetezi ndizo zinazoharibu ushahidi.
Wiki nne hazikuwa nyingi. Nilikuwa nimeshatolewa taarifa kwamba mimi ndiye nitakayekuwa shahidi wa kwanza wa upande wa serikali. Siku hiyo nikapanda kizimbani na kutoa ushahidi wangu.
“Ushahidi huo niliutoa kwa kuongozwa na wakili wa serikali. Ulianzia tangu nilipotaarifiwa juu ya kunyongwa kwa mtu wa kwanza, mtu wa pili, mtu wa tatu na mtu wanne.
Nilieleza jinsi nilivyofanya uchunguzi wa kunyongwa kwa watu hao.
Awali niliieleza mahakama kuhusu vipande vya karatasi ambavyo tulivikuta katika shingo za marehemu vikionesha alama ya dole ambalo tuliamini kuwa ni la muuaji pamoja na kuandika idadi ya watu aliowaua akianza na mtu wa kwanza hadi kuishia na mtu wanne.
Nilieleza jinsi nilivyopata namba ya simu ya mtu ambaye tuliamini kuwa ndiye muuaji na ghafla tukaja kugundua kuwa watu walionyongwa walishahukumiwa kunyongwa na mahakama miaka miwili iliyopita kwa kosa la mauaji.
“Tulivyofuatilia kwa mkuu wa gereza tukathibitishiwa kwamba watu hao walishanyongwa jambo ambalo lilitubabaisha kwa sababu ilishathibitika kwamba watu hao walikuwa hai na walinyongwa na mtu asiyefahamika,” niliieleza mahakama.
Nikaendelea kueleza kwamba katika uchunguzi wetu tulikuja kubaini kwamba wale watu walionyongwa hawakuwa wamenyongwa gerezani na kwamba mkuu wa gereza aliwatorosha ili kuwaepusha na adhabu ya kifo na badala yake alinyonga watu wengine kwa kutumia majina ya watu wale aliowatorosha.
“Uchunguzi wetu wa alama za vidole ulikuwa ukionesha kwamba aliyewanyonga ni mtu ambaye alishanyongwa. Alinyongwa na watu hao wanne na kusababisha washitakiwe kwa mauaji na kuhukumiwa kifo.
“Ikabidi twende tukafukue kaburi la huyo mtu aliyefahamika kwa jina la Thomas tuone kama tutamkuta kaburini.
“Kwa msangao mkubwa mwili wa mtu huyo tuliukuta kaburini lakini ukiwa na alama ya wino wa mhuri katika dole gumba lake. Alama hiyo ndiyo tuliyoikuta katika zile karatasi tulizozipata kwenye miili ya wale watu wanne walionyongwa.”
Nikaieleza mahakama kwamba hilo jamnbo liliishangaza polisi lakini tulikuja kumpata mzee mmoja ambaye alikuwa dereva wa baba wa hao watu walionyongwa ambaye alitufichulia mengi ambayo tulikuwa hatuyajui.
Nikatoa maelezo ambayo alitueleza mzee Mustafa wa Makorora kuhusu kadhia ya Unyeke na rafiki yake aliyemuachia mali na mtoto wake mpaka watoto wa Unyeke wakaja kumuua yule kijana ili wapate mali ambayo hawakustahili kuipata.
“Mheshimiwa jaji huyu mshitakiwa kama ambavyo alikiri kosa alijitokeza mwenyewe kituo cha polisi na kutueleza kuwa yeye ndiye aliyewanyonga watu hao kwa sababu walimuua ndugu yake. Yeye na Thoma ni shangazi kwa mjomba,” nikaeleza.
Baada ya kutoa maelezo yangu wakili wa mshitakiwa alisimama na kuniuliza nilithibitishaje kama kweli mshitakiwa ndiye aliyewanyonga watu hao.
“Alikiri mwenyewe bila kulazimishwa,” nikajibu haraka.
“Mmethibitisha kwamba yeye ndiye aliyewaua watu hao kwa kukiri yeye mwenyewe, hamna uthibitisho mwingine?”
Nilikuwa nafikiria jibu, wakili huyo akanibandika swali jingine.
“Kama leo angebadili kukiri kwake na kukana kosa angekuwa hana kosa?”
“Sasa kama yeye hakuua ni kwanini ajitokeze polisi na kukiri kwamba ndiye aliyewanyonga wale watu?”
“Mlimpima akili yake?”
“Hatukua na shaka na akili yake.”
“Wewe tangu umeanza kazi ya upelelezi ulishakutana na wahalifu wangapi ambao walijitokeza wenyewe na kukiri mbele yako kuwa wameua?”
“Kusema kweli huyu atakuwa mshitakiwa wa kwanza.”
“Kwa hiyo wewe hakukushangaza alipokwambia kwamba ndiye aliyewanyonga wale watu?”
“Bado hukuona kama kuna umuhimu wa kupima akili yake?”
Nikaamua kunyamaza baada ya kugundua ni kweli polisi tulifanya kosa kutokwenda kumpima akili mshitakiwa.
“Unakubali kwamba wakati mwingine mnafanya uzembe katika kazi zenu?” Wakili wa utetezi akaniuliza.
“Sikubaliani na hilo,” nikamjibu na kuongeza.
“Suala kama hilo halihusiani na uzembe. Inawezekana hatukuona umuhimu wa kupima akili yake kwa sababu hatukuwa na shaka naye. Tuliamini kwamba alikuwa mzima.”
“Sasa kama mliamini kwamba alikuwa mzima kwanini ulishangaa alipowambia kwamba aliwanyonga wale watu wanne?”
“Tulishangaa kutokana na umri wake mdogo na kule kukiri kwake bila wasiwasi kwamba alifanya kosa hilo.”
“Haiwezekani kwamba alikiri kosa ambalo hakulitenda kutokana na tatizo la akili?”
“Hatujui kama allifanya hilo kosa kutokana na tatizo la akili kama ulivyouliza.”
“Kwanini hamkwenda kumpima akili yake?’
Hapo nikanyamza kimya. Maswali yake yalikuwa yameanza kuzungusha akili yangu.
Mwendesha mashitaka akasimama na kumwambia mheshimiwa jaji.
“Wakili wa utetezi aeleze kama anataka mshitakiwa akapimwe akili. Hilo ni jambo dogo tu.”
Kabla ya jaji kusema lolote wakili wa utetezi akasema.
“Ndiyo. Nataka mshitakiwa akapimwe akili.”
Wakili wa serikali akasimama tena.
“Mheshimiwa jaji tunaomba uahirishe shauri hili ili mshitakiwa apelekwe katika hospitali ya wagonjwa wa akili kuchunguzwa akili yake kama upande wa utetezi ulivyotaka.”
“Ruksa mshitakiwa akapimwe akili yake. Unahitaji siku ngapi kwa ajili ya uchunguzi huo?” Jaji akamuuliza wakili wa serikali.
“Naomba uahirishe shauri hili kwa wiki tatu.”
“Sawa. Niinaahirisha shauri hili kwa wiki tatu kama ambavyo upande wa mashitaka umeomba ili mshitakiwa akafanyiwe uchunguzi wa akili yake.”
Shauri hilo likahirishwa kwa wiki tatu. Nikashuka kizimbani na kutoka nje ya mahakama ili kupata hewa safi. Jinsi mahakama ilivyokuwa imejaa watu, mapangaboi sita yaliyokuwa yamewekwa juu hayakuweza kutosha kuondoa fukuto ndani ya chumba cha mahakama.
Baada ya kuwa nje ya mahakama kwa karibu robo saa niliingia katika chumba cha mawakili na kuonana na wakili aliyekuwa akiendesha shauri la Faustin.
Tulijadiliana kuhusu kupelekwa hospitali kwa mshitakiwa Faustin ambapo tulikubaliana kwamba apelekwe hospitalini kesho yake.
Baada ya kuondoka mahakamani sikurudi ofisini. Nilikwenda kula chakula kwenye mkahawa mmoja. Baada ya kula chakula nilimpigia simu Hamisa.
Simu iliita kwa sekunde kadhaa bila kupokelewa. Nikakata simu na kupanga kumpigia wakati mwingine. Wakati nainuka kwenye kiti ili nitoke, Hamisa akanitumia meseji.
Nilipoifungua iliandikwa.
“Niko kwenye chumba cha upasuaji.”
Baada ya kuisoma ile meseji niliitia simu mfukoni nikatoka na kujipakia kwenye gari.
Zoezi la kumpeleka hospitali Faustin lilifanyika na tukapata majibu kwamba Faustin hakuwa na matatizo ya akili.