USAJILI inaofanya Yanga kupata wachezaji wa viwango vya juu katika madirisha ya miaka ya hivi karibuni, umemuibua mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Said Bahanuzi akiamini inaweza ikawa timu ya kwanza ya Tanzania kuchukua ubingwa wa Afrika.
Bahanuzi aliifafanua kauli yake amesema wakati Simba inachukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu minne mfululizo kuanzia 2017/18, 2018/19, 2019/20 na 2020/21 Yanga iliyumba, baadaye ikajisahihisha na kuanza kusajili wachezaji wa viwango vikubwa.
“Simba wakati inachukua ubingwa kipindi cha nyuma ilikuwa na wachezaji wenye viwango vikubwa wenye uwezo wa kuamua mechi, safu yao ya mbele alikuwepo Meddie Kagere aliyeibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo, Clatous Chama, Criss Mugalu, John Bocco, Luis Miquissone kwa kifupi walikuwa na uhakika wa kupata ushindi na ndiyo maana walikuwa wanafanya vizuri katika mechi za CAF,” amesema Bahanuzi na kuongeza;

“Yanga ikapokea kijiti cha kuchukua ubingwa kuanzia msimu wa 2021/22 hadi 2024/25 tangu hapo kikosi chao hata wakisajili hawawaachi wachezaji wao muhimu kwa mpigo, badala yake inatoa mtu inaingiza mtu wa kazi, hilo wakiendelea nalo siku moja litawafanya wachukue ubingwa wa CAF.
“Mfano baada ya kuondoka kwa Fiston Mayele aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao, jukumu hilo japokuwa walikuwa wanacheza nafasi tofauti akalibeba Stephane Aziz Ki msimu wa 2023/24, akaibuka kinara wa mabao 21 na asisti nane na wakati anaondoka 2024/24 alifunga mabao tisa, hivyo waliyopo bado wana uwezo mkubwa wa kufanya vitu vikubwa ambavyo vitawasaidia katika michuano ya CAF.”

“Bado Yanga imeendelea kusalia na kikosi cha watu ambao wana uwezo mkubwa wa kuamua mechi kama Maxi Nzengeli, Clement Mzize, Pacome Zouzoua na wengine wengi na ndiyo maana mechi za dabi Yanga imeifunga Simba mara nyingi, hivyo Simba irejee kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuamua mechi, mfano walipocheza fainali ya CAF dhidi ya RS Berkane wangekuwepo kina Kagere na Miquissone Simba ingechukua ubingwa.”

Bahanuzi aliyewahi kuandika rekodi ya kufunga mabao tisa katika michuano ya Kombe la Kagame mwaka 2012, amesema kwa kuwa Simba na Yanga zinatazamwa kama kioo katika michuano ya CAF zisajili majembe.”