KIUNGO mshambuliaji wa Konya Amputee inayoshiriki Ligi Kuu ya Walemavu nchini Uturuki, Ramadhan Chomelo amesema kuna asilimia 65 za kuondoka klabuni hapo baada ya kupata ofa kubwa kutoka timu mbili za ligi hiyo.
Msimu wake wa kwanza (2022/23) alicheza mechi 26 akifunga mabao saba na kutoa asisti 16, huku msimu wa 2023/24 akicheza mechi 21 na kufunga manne na kutoa asisti tisa. Msimu uliopita aliweka kambani mabao matano na kutoa asisti 11.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chomelo amesema kama atashawishika na ofa watakayomwekea Konya ataendelea kubaki, lakini kama mambo hayatakwenda sawa basi anaweza kutafuta changamoto sehemu nyingine.
“Ila kuna asilimia kama 65 za kuondoka hapa Konya. Kuna timu kama mbili zimeleta ofa nzuri, na kusema ukweli kikubwa watu tunaangalia pesa. Si unajua lazima tucheze kwa maslahi,” amesema Chomelo.
Kuhusu maandalizi ya msimu mpya amesema: “Kambini tunaingia Jumatano. Huwa hatuingii kambini sana kwa sababu wachezaji wa kigeni tumepangiwa nyumba, hivyo siku za mazoezi gari linatufuata tunaenda mazoezini.”
Mkataba wa Chomelo na klabu hiyo iliyomaliza nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi msimu uliopita unatamatika msimu huu, akiitumikia timu hiyo misimu mitatuo.
Kwenye Ligi ya Walemavu ya Uturuki kuna nyota watatu wa Kitanzania hadi sasa wanaokipiga katika timu mbalimbali. Ukiachana na Chomelo, yupo Shedrack Hebron wa Sisli Yeditepe na Mudrick Mohamed wa Mersin.