DKT.SAMIA:KIPAMBAUMBELE CHETU KATIKA SEKTA YA MADINI KUWAWEZESHA WACHIMBAJI WADOGO

 Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika sekta ya madini mkakati wa Serikali katika miaka mitano ijayo ni kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo ikiwemo kuwapatia mitambo ya uchorongaji.

Akizungumza leo Oktoba 11,2025 katika mkutano wa kampeni kuomba kura kuelekea Uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu uliofanyika wa Kambarage uliopo Kahama Mjini mkoani Shinyanga Dk.Samia amesema katika sekta ya madini Serikali itaendelea kuliwezesha kundi la wachimbaji wadogo kama ilivyo mwaka jana.

“Kama ambavyo tulivyofanya katika kipindi hiki ndivyo ambavyo tutaendelea katika miaka mitano ijayo katika kuwainua wachimbaji wadogo.

“Lakini jingine ni kupima maeneo yetu utafiti kwa kutumia teknolojia ili tujue kwa uhakika tunamali kiasi gani, maeneo gani na ni madini gani yako wapi lakini kipaumbele chetu ni vijana wetu wachimbaji wadogo .Hatutaweza kuwaepuka wawekezaji wakubwa lakini kipaumbele cha nchi ni wachimbaji wadogo.

Kuhusu sekta ya elimu Dk.Samia amesema kuwa pamoja na kuendelea na kuboresha sekta hiyo kwa kujenga miundombinu ya shule za msingi,Sekondari na vyuo vya VETA lakini Serikali inatambua wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule zao , vifaa vyao na mambo yao yote.

“Tutaendelea kutoa kila kinachohitajika wa wanafunzi wenye uhitaji ili nao waingie kusoma elimu wawe kama wenzao.Pamoja na kutekeleza sera za ndani ya nchi yetu pia tutatekeleza matamko ya kimataifa yanayotutaka tusimwache mtu yeyote nyuma sasa kila mwanadamu tuna wajibu kuhudumia vile mungu alivyomleta duniani.”

Kuhusu Viwanda amesema katika Mkoa wa Shinyanga na Wilaya ya Kahama amoena mahitaji ya viwanda na  katika miaka mitano iliyopita Serikali imejitahidi  kuendeleza kongani za viwanda na itaendelea na kazi hiyo.

“Tutaleta umeme wa kutosha ili tuwe na viwanda utumike kwenye viwanda. Tayari tunatayarisha watumishi, wafanyakazi kuja kwenye viwanda kupitia vyuo vya ufundi na lengo ni kuvutia viwanda.

Ametoa rai kwa mikoa na Wilaya kujenga mazingira mazuri wakati Serikali Kuu ikiendelea kujenga mazingira mazuri ya kisera na kisheria na kikodi lakini katika mikoa kujenga mazingira mazuri kupokea wawekezaji vijana wapate ajira.