Dodoma. Daniel Goleman, mwandishi wa kitabu cha Emotional Intelligence, aliwahi kusema, “Usipomsaidia mtoto kujenga umahiri wa kuelewa na kumudu hisia zake, unamwandaa kuwa mtu atakayepata shida kwenye uhusiano wake na watu.
Malezi, kwa msingi huo, yanalenga kushughulika na hisia za mtoto.” Hapa ninakuletea njia tano za kujenga umahiri wa mtoto kumudu hisia zake.
Wapo watoto wasioelewa wanajisikiaje. Ukimwuuliza anajisikiaje ataishia kukuambia, “Ninajisikia vibaya”, “Najisikia vizuri.” Mtoto asiyejua anajisikiaje ataishia kuficha hisia zake na hivyo kutengeneza tatizo la kupelekeshwa na hisia.
Msaidie mtoto kutambua anajisikiaje.
Huu ni mchakato muhimu kwa mtoto tunayetaka ajue kumudu hisia zake. Je, anajisikia aibu, fedheha, furaha, huzuni, woga, fahari, hatia na kadhalika?
Katika mazoezi ya kutambua hisia, nimebaini watu hupata tabu kutofautisha hisia na tafsiri ya kile wanachofikiri.
Mfano, ukisema, ‘najisikia kupuuzwa’, hayo ni mawazo yako na sio hisia. Kupuuzwa sio hisia ni tafsiri. Huenda umejisikia unyonge na wala hakuna mtu amekupuuza. Kutambua unajisikiaje ni jambo la msingi.
Kwa nini tuna hisia? Hisia zina kazi gani? Kwa nini unajisikia woga, haya, fedheha, upendo na kadhalika? Kila hisia ni jaribio la mwili kukusaidia kumudu mazingira.
Muhimu kuelewa kuwa nyuma ya kila hisia kuna hitaji fulani. Mtoto anapojisikia uoga, mathalani, maana yake alihitaji usalama, aone vitu kama vinatabirika. Mtoto anapoona dalili za kukosekana usalama huo, uoga unakuwa ni matokeo.
Mfundishe mtoto kuwa hakuna hisia mbaya. Unavyojisikia si tatizo bali tabia inayosababishwa na hisia hiyo. Kukasirika, kwa mfano, hakuwezi kuwa tatizo. Kuumiza mtu kwa sababu umekasirika hilo ndilo tatizo.
Mtoto aelewe kwa nini anajisikia hasira. Kujisikia hasira maana yake kuna hatari ameiona inayotishia usalama wake. Hasira inalenga kumfanya apambane na hatari hiyo. Uoga, tofauti na hasira, inakuja kama namna ya mwili kuikimbia hatari. Hakuna ubaya kujisikia woga au hasira.
Ipo haja ya kuwafundisha watoto kuelewa kwa nini wanajisikia vile wanavyojisikia.
Unaweza kuelewa hisia zako lakini usiweze kuzibaini kwa mtu mwingine. Kwa hivyo, ni muhimu kwa watoto kujifunza kubaini hisia za watu wengine. Jambo hili si jepesi lakini linawezekana.
Ili kujifunza kubaini hisia, ni muhimu mtoto kujifunza msamiati wa kutosha kuelezea hisia za mtu mwingine. Kwa mfano, unaweza kumsaidia kutumia msamiati sahihi kubaini mwenzake anajisikiaje.
Mfano watoto wamekuja kushitakiana kwa ugomvi. Kila mmoja analalamika vile alivyotendewa. Hapa unaweza kumtaka kila mmoja kuelezea vile mwenzake anavyojisikia.
‘Unadhani Maulidi alijisikiaje ulipoondoka na mdoli wake?’ Kuza msamiati wake kwa kumsaidia kutaja hisia ya mwenzake. ‘Maulidi alikasirika. Hasira ikamfanya akusukume.’ Faida kubwa ya kubaini hisia ni kumfanya mtoto aelewe hisia za wengine.
Tumelelewa kuficha hisia zetu. Ukikosana na mtu unaonekana una hekima ukiweza kuigiza kutokuwa na maumivu. Hatari yake ni kwamba hisia zisipooneshwa kuna mahali zinafukiwa kwenye ufahamu na hiyo inaweza kuwa hatari kubwa mbele.
Tumeshuhudia watu wanaolipuka kwa hasira wakati mwingine kwa vitu vidogo. Tumeshuhudia watu wanaoogopa hata vitu wasivyopaswa kuviogopa. Moja ya sababu ni kufukia hasira.
Tunaweza kuwafundisha watoto namna bora ya kuonesha hisia bila kuleta madhara. Mfano, ukikasirika, unaweza kuelezea hasira zako kwa lugha isiyolaumu.
Kumudu hisia ni ule uwezo wa kudhibiti namna unavyoonesha hisia kulingana na mazingira. Kuna wakati wa kuonesha hisia kama zilivyo, kuna wakati wa kuzuia hisia hizo kidogo na kuna wakati ni muhimu kuziachilia kwa kiwango fulani.
Mtoto aliyefundishwa kumudu hisia anajiongezea uwezekano wa kutogombana na wenzake.
Mfano tunaweza kuwafundisha watoto kutosema sana wanapokuwa na hasira. Unapozungumza ukiwa na hasira unaweza kufanya kitu utakachokijutia baadaye.
Kuna wakati ukinyamaza wakati mwenzako amekasirika, unaweza kutafsirika kuwa na kiburi na ukampandisha mwenzako hasira. Unasema nini unapokuwa umemkasirisha mwenzako hicho nacho ni kipimo cha ukomavu wako wa kihisia. Badala ya kujitetea au kunyamaza, kuomba msamaha kunaweza kuwa hekima kubwa.