Dar es Salaam. Wakati ikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imefanya marekebisho katika maeneo ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 ikiwemo kuzifuta kata 10, kutengua na kuwaondoa wagombea udiwani saba.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumapili Oktoba 12, 2025 na kusainiwa na Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele, uamuzi huo umefikiwa baada ya tangazo la Serikali Na. 596 namba 600 la Oktoba 3, 2025, ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) alitangaza marekebisho ya mipaka ya maeneo ya utawala na kufuta kata kadhaa.
Kwa mujibu wa INEC, kata zilizofutwa ni Litapunga, Kanoge, Katumba, Mishamo, Ilangu, Bulamata, Ipwaga, Milambo, Igombemkulu na Kanindo.
Aidha, tume imetengua uteuzi na kuwaondoa katika orodha ya wagombea udiwani saba walioteuliwa katika kata husika ambao wote kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Salehe Mrisho Msompola (Kata; Kanoge), Elius Wilson Elia (Kata: Katumba).
Wengine ni Mohamed Ally Asenga (Kata: Litapunga), Nicas Athanas Nibengo (Bulamata), Sadick Augostino Mathew (Ilangu), Rehani Simba Sokota (Ipwaga) na Juma Mohamed Kansimba (Mishamo).
Taarifa hiyo imeeleza kuwa INEC imelazimika kufuta vituo 292 vya kupigia kura vilivyokuwa kwenye kata zilizofutwa.
“Tume imeanzisha vituo vipya 292 vya kupigia kura katika kata jirani na kata zilizofutwa kuwawezesha wapigakura kutoka katika maeneo yaliyofutwa,” imesema INEC.
Ikieleza zaidi INEC imeeleza wapiga kura 106, 288 waliokuwa kwenye vituo vilivyofutwa wamehamishiwa kwenye vituo 292 vya kupigia kura vilivyoanzishwa kwenye Kata za Mtapenda, Uruwira, Nsimbo, na Ugala zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo mkoa wa Katavi.
“Kata nyingine walizohamishiwa ni Sasu, Ilege, Uyowa, Makingi na Silambo zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoa wa Tabora na Kata ya Tongwe iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Katavi,” imeeleza taarifa hiyo,
Aidha tume imetoa wito kwa wananchi kuzingatia mabadiliko hayo ya maeneo ya uchaguzi ili waweze kutumia haki yao ya msingi kushiriki kupiga kura siku ya uchaguzi.
