JENISTA MHAGAMA_ AIPONGEZA SERIKALI YA CCM KUBORESHA SEKTA YA ELIMU, UFAULU WAONGEZEKA JIMBO LA PERAMIHO

 Mgombea ubunge wa Jimbo la Peramiho Halmashauri ya Wilaya ya Songea kupitia CCM  na Waziri wa Afya Jenista Mhagama, amesema kiwango cha ufaulu kimepanda kutokana na juhudi za serikali ya Chama cha Mapinduzi kuboresha sekta ya elimu.

Akiwa kwenye kampeni kijiji cha Lipokela Kata ya Mbinga_Mhalule, alisema madarasa mapya yameanza kujengwa, shule shikizi imeanzishwa katika maeneo ya Mbinga Road, na shule ya sekondari Lipokela itakamilika kupitia Ilani ya uchaguzi ya 2025–2030 ili wanafunzi wote wapate elimu bora maeneo yaliyo karibu.

Serikali imejipanga kuongeza idadi ya walimu na kuboresha miundombinu ya shule kwa kujenga zaidi ya madarasa 250 na vyoo 150 katika maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo, vikiwemo vijiji vya Mscheke, Mbinga Road na Lipokela, alieleza kuwa sera mpya ya elimu itasimamia kwa karibu viwango vya ufaulu na kuhakikisha kila mtoto anapata mazingira bora ya kusomea.

Mbali na elimu, Jenista amesema serikali imetekeleza miradi ya umeme katika vijiji vilivyokuwa havijaunganishwa mwaka 2020, na maeneo yaliyobaki yako kwenye mpango wa kuunganishwa ambayo ni ngazi ya vitongoji, Aidha, serikali imetenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa barabara zinazounganisha vijiji vya Nakahegwa, daraja kuelekea Litisha pamoja na ujenzi wa vivuko vya kudumu vinavyopitika mwaka mzima.

Katika sekta ya afya, ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Lipokela umekamilika na kuahidi kuwa serikali ya CCM itaendelea kuboresha huduma za afya vijijini kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya.

Jenista pia ametaja ajenda ya uchumi jumuishi kupitia utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana, na wakulima, makundi maa sambamba na kuendeleza ruzuku ya mbegu na mbolea ili kuongeza tija katika kilimo. Ameishukuru taasisi kama Shamba la Aviv kwa ushirikiano katika kutekeleza miradi ya kijamii kijijini hapo.

Amewaomba kura za ndiyo za kishindo kwenye uchaguzi ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 kuanzia ngazi ya Udiwani, Ubunge na Urais kwani kwa kuichagua CCM ni kuchagua maendeleo ya kweli.