Kapilima ajiweka kando KenGold | Mwanaspoti

ALIYEKUWA Kocha wa KenGold, Omary Kapilima amesema kwa sasa amejiweka kando na timu hiyo iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Championship, baada ya kukifundisha kikosi hicho cha jijini Mbeya rasmi tangu, Oktoba 22, 2024.

Kocha huyo aliyewahi kuchezea na kufundisha timu mbalimbali zikiwemo Majimaji, Yanga na Mtibwa Sugar, alijiunga na kikosi hicho Oktoba 22, 2024, baada ya Fikiri Elias, kuondoka Septemba 17, 2024, kwa makubaliano ya pande zote mbili.

“Nimeamua kupumzika kwanza kwa sasa baada ya kipindi kirefu kilichobeba changamoto nyingi, ni uamuzi wa kwangu binafsi, ingawa muda siyo mrefu mashabiki na wadau wangu wataniona tena nikiwa na timu nyingine hivi karibuni,” amesema Kapilima.

Timu hiyo iliyocheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, ilianza kufundishwa na Kocha Fikiri Elias, kisha kuteuliwa Omary Kapilima akisaidiana na Jumanne Challe waliyeiongoza hadi mwisho mwa msimu, licha ya ujio pia wa Mserbia Vladislav Heric.

Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.

Licha ya kiwango hicho, ila KenGold ilishindwa kumudu presha za Ligi Kuu na msimu wa 2024-2025 iliburuza mkia na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 23.