KOCHA Mkuu wa Gunners ya Dodoma, Juma Ikaba amesema mojawapo ya vipaumbele vyake kwa timu hiyo msimu huu, ni kuhakikisha kikosi hicho kinapanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027, japo ikishindikana basi waendelee kubakia Ligi ya Championship.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ikaba amesema licha ya ubora wa nyota wa timu hiyo ila hataki kuwapa presha zaidi kutokana na ushindani uliopo, ingawa ugeni wao sio kigezo cha wapinzani kuwabeza, kwa sababu wana uwezo na nia ya kufanya chochote.
“Kitu cha kwanza tulichofanya ni kuongeza wachezaji watatu hadi wanne wazoefu wanaoweza kutusaidia, lengo ni kuhakikisha hatuvurugi balansi ya timu kwa maana ya uchezaji wetu, tumejipanga vizuri na tupo tayari kuonyesha hilo,” amesema Ikaba.
Gunners imepanda Ligi ya Championship msimu huu, baada ya kuongoza First League kundi B na pointi 35, kufuatia kushinda mechi 11, sare miwili na kupoteza mmoja, ikiungana na kikosi cha Hausung kutoka Njombe iliyoongoza kundi A na pointi 25.
Baada ya timu hizo kuongoza makundi yao na kupanda Championship, zilicheza mechi ya fainali kusaka bingwa mpya wa First League kwa msimu wa 2024-2025 na kikosi hicho cha Gunners kilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Hausung mabao 3-0.