Magdalena Shauri avunja rekodi, Kiplimo akitwaa medali ya dhahabu

Bingwa wa marathoni wa Tanzania kwa upande wa wanawake, Magdalena Shauri, ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya taifa baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika mbio za Chicago Marathon zilizofanyika leo Jumapili Oktoba 12, 2025 nchini Marekani, na kuvunja rekodi yake binafsi ya muda wa mbio ndefu.

Shauri, ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya muda wa saa 2:18:41 aliyoiweka mwaka 2023 kwenye Berlin Marathon, ameonyesha ubora na uthabiti mkubwa kwa kuvunja rekodi hiyo leo baada ya kukimbia kwa saa 2:18:03, akiboresha muda wake kwa sekunde 38.

Kwa matokeo hayo, nyota huyo kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), amethibitisha kuwa ni miongoni mwa wanariadha bora zaidi duniani kwa sasa katika marathon, akiweka historia nyingine muhimu kwa Tanzania katika mashindano ya hadhi ya juu duniani.

Wakati huohuo, Hawi Feysa kutoka Ethiopia ndie ameibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake katika mbio hizo baada ya kutumia saa 2:14:56, akifuatiwa na mwenzake Megertu Alemu kwa 2:17:18 huku Loice Chemnung wa Kenya akimaliza wa nne kwa 2:18:23.

Kwa upande wa wanaume, Jacob Kiplimo ameshinda mbio hizo kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake kwa muda wa saa 2:02:23, ikiwa ni mbio yake ya pili tu katika masafa ya kilometa 42.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 24 kutoka Uganda, alionyesha ubabe mkubwa baada ya kujitenga na bingwa mtetezi wa Chicago na Boston, John Korir, muda mfupi baada ya kupita nusu ya njia kwa muda wa saa 1:00:16.

Kiplimo alimaliza mbio hizo akiwa sekunde 91 mbele ya Amos Kipruto aliyetumia 2:03:53 huku Mkenya mwenzake Alex Masai akimaliza katika nafasi ya tatu kwa 2:04:37, ambapo Korir yeye maji yalizidi unga na kushindwa kumaliza mbio.

Mmarekani Conner Mantz alimaliza wa nne na kuvunja rekodi ya taifa ya Marekani iliyodumu kwa miaka 23 iliyokuwa ikishikiliwa na Khalid Khannouchi, baada ya kuvuka mstari wa mwisho kwa muda wa 2:04:43, akipunguza sekunde 57 kutoka rekodi ya zamani.

Kiplimo alianza kushiriki marathon mwezi Aprili 2025 jijini London, ambapo alikimbia kwa muda wa 2:03:37 na kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Sebastian Sawe, lakini leo katika mbio za Chicago, alionekana kwa muda mrefu kuwa kwenye kasi ya kutishia kuvunja rekodi ya dunia iliyowekwa na marehemu Kelvin Kiptum.

Kiptum, ambaye alifariki kwa ajali ya gari akiwa na umri wa miaka 24 miezi michache tu baada ya kuweka rekodi ya dunia, alikimbia muda wa 2:00:35 kwenye Chicago Marathon mwaka 2023, muda ambao bado unashikilia rekodi ya dunia hadi sasa.